Aliyoyasema KK bungeni
.
{Mauaji ya Mwembechai 1998}
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana
Mheshimiwa Spika. Mbunge mwenzetu wa Jimbo la Ukerewe ana maneno ambayo
huyasema mara kwa mara.Ni maneno ya busara na mimi ningeomba niyanukuu hapa leo.
Anasema hivi "Simple minds discuss people…ordinary minds discuss events…..great
minds discuss ideas" (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Nabii Mussa Alayhis-Salaam alipopewa kazi ya kwenda
kuwarudisha Mayahudi kule Misri alimwambia Mungu "Ewe Mola wangu mimi nina
kigugumizi, kazi hiyo siiwezi peke yangu nakuomba unipe Haroun anisaidie". Mungu
akampa na kazi ikafanyika. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kuna methali ya Kiswahili inayosema "Kikulacho kimo nguoni
mwako". Kuna methali ya Kiswahili inayosema "Laumu ulikojikwalia, usilaumu
ulikoangukia". (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni mimi nilifanya Press Conference kule
Dar es Salaam. Katika Press Conference yangu nilisema niliwaomba Polisi
waache kuwashtaki Waislamu kwa kosa la kusema "Yesu si Mungu". Kwa sababu maneno
yale yamo ndani ya Qur-an. Kama kwa bahati mbaya Waislamu hao wakipata
‘conviction’ itabidi I proscribe dini ya Kiislamu, wanaiona hatari yake.
Nikawaomba pia Polisi wawape dhamana hawa watu maana yake waliokuwa wakipiga
kelele wasipewe dhamana, wasipewe dhamana ni Polisi, wapewe dhamana hawa watu.
Baada ya siku chache Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani akatoa kauli akasema
Mbunge anayo haki ya kutoa fikra zake, lakini baadaye Waziri mwenyewe akatoa
kauli akasemaMbunge anatafuta umaarufu. Hili suala la umaarufu katika kitabu
hiki Waziri amelitaja mara tatu. Sasa kwanza mimi nataka nimwambie Waziri kwamba
mimi sitafuti umaarufu Dar es Salaam.Mimi Dar es Salaam maarufu. Mimi Dar es
Salaam nina wastaha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika,katika maisha yangu yote nimekuwa msema kweli na wewe
unajua. Nimekuwa msema kweli kwa kiongozi wa Awamu ya Kwanza, mbele yako,
nimekuwa msema kweli kwa Kiongozi wa Awamu ya Pili na nimekuwa msema kweli kwa
Kiongozi wa Awamu hii. Sasa kama kusema kweli kwa viongozi wako ndiyo
kulitakiaTaifa mabaya basi chama changu kitanihukumu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nataka nirudie tu niliyoyasema na
nipate maelezo kutoka kwa Waziri. Hivi karibuni hapa Dodoma askari
wawiliwaliacha malindo yao wakaadhibiwa kwa kufukuzwa kazi. Nilipochangia hoja
ya Waziri Mkuu niliuliza habari ya Chuki Athumani amekaa na pingu miezi minne na
hakufunguliwa pingu ingawa Rais alimpa ruhusa alitoa amri aachiliwe,
Mheshimiwa
Waziri Mkuu alikubali kwa naam". Chuki amekaa miezi minne na hakuachiliwa mpaka
Waziri mwenyewe alipokwenda Dar es Salaam tarehe 17/6/98. Sasa mimi ninachotaka
kujua kama hawa askari wawili hawakukaa kwenye malindo wamefukuzwa, wale ambao
waliokiuka na kukataa kufuata amri ya Rais wamefanywa nini. Ni kina nani hao?
Narudia kule kule kwa uwazi na ukweli. Ningeomba Waziri aseme anaogopa nini
kwani na yeye anahusika. Amri imetolewa na Rais, watoto wote watolewe pamoja na
Chuki Athumani. Chuki amekaa miezi minne gazeti la Observer linasema kama
angetolewa wakati ule huenda hali yake isingekuwa kama ilivyo sasa. Sasa tujue
Imam wa Msikiti Bet-il-Mukadas, Mussa Katambo ana umri wa miaka 83. Rais amesema
atolewe, amekaa mahabusu miezi mitano ametolewa juzi tu na hajulikani hivi sasa
kama ataishi au atakufa. Imam wa Msikiti wa Kinondoni Mtambani,Chata Abdallah
ana umri wa miaka 78 amekaa ndani miezi mitano hakutolewa mpaka juzi wiki
iliyopita. Ninachotaka kujua, sitaki mimi kujua, wengi wanahitaji kujua. Umma wa
Watanzania wanataka kujua, je waliohusika nakukataa amri ya Rais ni kina nani,
wamefanywa nini au watafanywa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hawa ambao hawakutekeleza wajibu wao ndio wasiolitakia mema
Taifa letu. Kwa sababu kama wale Maimam wangefia jela ghasia zake zisingekuwa
ndogo, hivyo Waziri halijui hilo.
Sasa la pili nataka kulisema hili jambo la "Yesu si Mungu". Cardinal wa
Kanisa Katoliki Pengo amesema ya kwamba kwa Muislamu kusema Yesu si Mungu si
kashfa dhidi ya Ukristo na ameendelea kusema kwamba kwa Mkristo kusema ya kwamba
Muhammad si Mtume wa mwisho si kashfa kwa Muislamu. Ma-Bishop wa Pentecosti
wamesema hivyo hivyo. Sasa kwa nini Polisi walikuwa wakiendelea kukamata watu,
kuwashtaki kwa kosa hilo hilo, dhidi ya dini nyingine, dini gani tena. Dini ndio
hizo, Catholic na Prostestant wote wanasema si kosa. Sasa hawa ndio wasioliombea
Taifa letu mema. (Makofi)
Mheshimiwa Spka, kama ujuavyo babu zangu, babu yangu mmoja hapa na wengine
wamesaidia sana alhamdullilah. Rais akawatoa wote wale. Leo Dar es Salaam hakuna
tena mtuhumiwa wa kesi za Mwembechai aliyekuwa mahabusu na wachache waliobakia
wameshatolewa kwa dhamana. Lakini msikitini Mwembechai kuna askari juzi nakuja
huku nimewakuta 14 wengine wana bunduki, jana nimepiga simu naambiwa wako tisa
na bunduki wanalinda nini. Mahakimu wanasema ya kwamba mambo haya yamekwisha
ndiyo maana wakawapa dhamana hawa. Sasa wale askari waliokuwa Mwembechai mpaka
leo na bunduki wanalinda nini. Waislamu wa pale wanasema wanawazuia Waislamu
wasisali kwa sababu mle ndani kulikuwa na darasa la watu wazima, kulikuwa na
darasa la wanawake na kulikuwa na madrassa ya watoto hakuna kwa sababu ya
kuogopa askari.
Mheshimiwa Spika, tuambiwe basi, siku ya Ijumaa msikiti ule ulikuwa unajaa
watu tele ndani, nje unajaa. Leo wanaosali katika msikiti ule safu mbili, safu
kwa Wasukuma, Wanyamwezi na Wadigo wasioelewa maana ya safu ni mistari. Mistari
miwili siku ya Ijumaa mistari minne, jumla sita, sababu ya kuogopa askari. Sasa
ningeomba Wziri atueleze kama Mahakimu wanasema pale ghasia imekwisha, Rais
ametoa watu wote wale askari pale mpaka leo wanafanya nini?
Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la parole nataka nimwambie Waziri kwamba
"Kikulacho kimo nguoni mwake". Hiyo kengele? Lahaula!! Parole watu wake Waziri
wamempelekea majina ya jamii moja. Waziri atanabahi akayakubali,akamshawishi na
Waziri Mkuu kwenda kuzindua. Baraza Kuu na Taasisi za Kiislamu wamepiga kelele.
Rais amefuta akamwambia aunde upya akizingatia uwiano wa jamii. Sasa mimi nasema
wale waliombambikia yale majina ndio wasiolitakiaTaifa mema. (Makofi)
Sasa Waziri anasema ya kwamba kazi hiyo ataifanya katika kipindi cha mwaka
1998/99. Kazi iliyokuwepo ni kupunguza katika wale ishirini wa jamii moja
akapunguza akaweka wengine wa jamii nyingine ni kazi ya siku mbili. Inakuwaje
ichukue mwaka mzima. Sasa ndiyo namwambia tufuate mfano wa Nabii Mussa kama yeye
hawajui hao wa jamii nyingine wenye elimu ya kutosheleza kuwa wenyeviti arudi
kwa bwana mkubwa. Bwana wewe umenipa kazi hii lakini hii jamii nyingine siwajui
waliosoma kiasi hiki,utampa Haroun. (Makofi/Kicheko).
Mheshimiwa Spika, nimesema mwaka jana kwamba mimi ni askari wa zamani kwamba
nalipenda sana jeshi langu. Lakini ni wajibu wa mtu yoyote kama unampenda mtu
umwambie kweli. Polisi hivi sasa wana makosa, nitoe mfano wamekwenda kumkamata
Magezi msikiti wa Mwembechai baada ya salat alasiri, watu wamejaa pale.
Walikazania nini kama siyo ghasia? Wamekwenda kumkamata Ponda Issa Ponda,
baada ya swalat I-jumaa ikatokea ghasia. Walitazamia nini? Hawa Masheikh wengine
walikwenda kuwakamata nyumbani hakuna ghasia iliyotokea. Wamekwenda kumkamata
Bishop Mugala kule Kurasini ndani ya kanisa. Taadhima gani hii? Kwa bahati nzuri
waumini wake wakaanza kuimba nyimbo za dini. Lakini kuna wengine hawaimbi nyimbo
za dini, hawakubali. Sasa mimi nasema Waziri ajue kwamba hawa wanaowasema
wasiolitakia Taifa mema anao. Mimi tabia yangu husema kweli na sisemei
uchochoroni. Ninapokuwa na jambo nakwenda kwa Kiongozi wangu, namwambia
niliyokuwa nayo.Inawezekana nikakosea. (Makofi).
Sasa kama kwa kusema kweli, kumwambia kiongozi wako ni kukosa kulitakia mema
Taifa, basi chama changu na serikali yangu wataamua. Lakini nitaendelea kufanya
hivyo kila ninapolipata neno. Nilikuwa nikifanya hivyo katika awamu ya kwanza,
katika awamu ya pili na nitafanya hayo katika awamu ya tatu. Tuzungumze kama
anavyosema huyu Mbunge mwenzangu wa Ukererewe kwamba tuzungumze ideas. Let us
not discuss people; let us not discuss events; let us discuss ideas. Hili lipo
tulifanyeje. Watu wananung’unika Mwembechai. Watu wameuawa. Waziri kasema
atafanya uchunguzi mpaka leo hakuna uchunguzi. Hapa anatueleza maneno mengi.,
ameyapata wapi?
Mheshimiwa Spika, nasema na nimesema mara nyingi kwamba nchi hii hakuna
ghasia za kidini. Kuna ghasia zinazoonyesha insensitivity ya askari wake. Sasa
ningemwomba Waziri leo afanye kama vile wanavyofanya kwa wengine. Kama kulikuwa
na Tume mbili za kuchunguza ghasia za Arumeru ambako hakufa hata mtu mmoja, kama
kulikuwa na shughuli za kelbu, mbwa, immigration, mpaka Jaji Mkuu akatoa kauli,
aunde Tume ya kuchunguza mauaji ya Mwembechai. Halafu ile Tume impe ripoti na
ripoti ya Tume ile ndiyo ailete atuambie Tume imeniambia hivi na hivi. Kukosa
kufanya hivyo ni hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, muda wenyewe umekwisha. Kengele sijaisikia. Niongee dakika
moja.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wangu umekwisha nataka kusema kwamba naunga
mkono hoja ya Waziri lakini natazamia kwamba haya niliyomwuliza atayajibu kwa
sababu yapo katika manufaa yake, manufaa ya Taifa na manufaa yetu wote.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi).
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !