Nchimbi atema cheche mihadhara ya kidini. - Kitoloho
Headlines News :
Home » » Nchimbi atema cheche mihadhara ya kidini.

Nchimbi atema cheche mihadhara ya kidini.

Written By Msamaa on Friday, May 10, 2013 | 12:52 PM

Amewaagiza makanda wa polisi wa mikoa yote nchini, kuhakikisha kuwa mihadhara haiendshwi.

Dar es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amepiga marufuku mikutano ya hadhara isiyokuwa na vibali maalumu vya vyombo vya dola.

Kauli hiyo imekuja siku moja baada ya viongozi wa dini, kutaka mikutano ya hadhara isifanyike bila kufuata taratibu za kisheria.

Waziri Nchimbi pia amewaagiza makamanda wa polisi kote nchini, kuwafuatilia kwa karibu watu watakaokiuka agizo hilo na kuwachukulia hatua za kisheria.
Dk Nchimbi alitoa agizo hilo juzi usiku jijini Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza katika mkutano wa viongozi wa dini.

“Kuanzia sasa sitaki kusikia eneo fulani kuna uvunjifu wa amani kwa sababu ya masuala ya imani za dini,” alisema waziri.

Alisema kamanda yeyote wa polisi atakayeshindwa kudhibiti tatizo hilo, atakuwa wa kwanza kuwajibika katika eneo lake la kazi.

“Serikali imechoshwa na vitendo vya uvunjifu wa amani, kumeanza kujitokeza makundi ya watu wasioitakia mema nchi kwa kusambaza sumu ya chuki kwa Watanzania,” alisema.

Akizungumza kwa hisia kali, Dk Nchimbi alisema si vizuri wanasiasa kueneza chuki kwa kutumia viongozi wa dini kwa sababu kuna siku chuki hizo zitakuwa mbaya kwa taifa.

“Kupitia mkutano huu naomba maaskofu, wachungaji na masheikhe, msikubali kupandikiziwa mbegu za chuki na wanasiasa wanaojitafutia umaarufu kupitia dini,” aliongeza.

Akizungumzia kusambaa kwa maneno ya uchochezi kupitia mitandao ya kijamii alisema: “Ninaomba wazazi tuwaonye watoto wetu na vijana wetu wanaotumia mitandao hiyo vibaya kwani kama itaendelea kuachwa itumike ovyo, itaharibu amani tuliyokuwa nayo kwa zaidi ya miaka 50,” alionya Nchimbi

Katika hatua nyingine, alibainisha kwamba kwa sasa Serikali na vyombo vya usalama vinafuatilia mawasiliano ya simu yanayofanyika hasa yanayolenga kueneza masuala ya udini.

“Nataka niseme kwamba tutachukua hatua kali za kisheria kwa watu wanaotuma na kutengeneza meseji zinazoeneza udini na kujenga chuki kwa Watanzania na sasa tumeanza kuzifuatilia,” aliongeza.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alisema wamefikia maazimio 16 yaliyotokana na kikao cha majadiliano ya viongozi wa dini huku kubwa likiwa kudumiasha amani ya mkoa huo na taifa kwa jumla.

Maazimio hayo ni kutokuruhusu amani kuchezewa, viongozi wa dini wajihadhari na matamko yanayoweza kuleta mfarakano miongoni mwa jamii na waheshimu imani za wengine.

SOURCE: MWANANCHI{10/05/2013}
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template