JK: Wanaovuruga amani wana uhusiano na mataifa ya nje. - Kitoloho
Headlines News :
Home » » JK: Wanaovuruga amani wana uhusiano na mataifa ya nje.

JK: Wanaovuruga amani wana uhusiano na mataifa ya nje.

Written By Msamaa on Sunday, May 19, 2013 | 12:45 PM


RAIS Jakaya Kikwete amesema Watanzania wanaoivuruga amani nchini wana uhusiano na watu kutoka mataifa ya nje. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jana, wakati akizungumza katika misa ya kutawazwa kwa Askofu Mkuu wa sita wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya. Alisema iwapo vurugu za kidini zitatokea, watu hao wakati wowote watakimbilia nje ya nchi.
“Tusivuruge amani ya nchi yetu, kwa kuwa ikivunjika hatuna pa kwenda, hao wanaovunja amani wanao uhusiano nje ya nchi, ikitokea vurugu tu wanakimbilia huko, wanakuwa wanatoa matamko huko waliko,” alisema.

Aliwataka viongozi wa dini kuliombea taifa ili wale wenye dhamira mbaya za kutaka kuwagombanisha Watanzania kwa dini zao wabadilike.

“Inasikitisha kuwa baadhi ya watu hawapendi kuona Watanzania wakiishi kwa amani na utulivu bila kujali itikadi za dini, rangi wala makabila kama ambavyo tumezoea.

“Wao usiku na mchana wanafanya kila mbinu wawafanye watu wagombane kwa misingi ya dini, Serikali haitakubali hilo litokee, imejizatiti kwa watu hao wenye dhamira mbaya.

“Kamwe hatutaacha kuwachukulia hatua, hatutachoka na tutawafikisha katika vyombo vya sheria, hatumwonea mtu, bali tutachukua hatua kwa wale wanaostahili,” alisema Rais Kikwete.

Aliwataka pia viongozi wa dini kufanya ibada zao bila kukashifu dini nyingine na kwamba ukitaka mtu akufuate siyo lazima ubeze dini nyingine.

“Acheni maneno ya kukashifu dini nyingine, jichungeni wenyewe ili kusiwe na ulazima wa kila mkusanyiko wa kidini, Serikali ije iwalinde,” alisema.

Alisema dini zote duniani zinahubiri upendo na amani na kwamba hakuna dini inayohubiri kuua, isipokuwa dini ya shetani peke yake.

Alisema kuruhusu uhuru wa kuabudu isiwe sababu ya kutukanana na baadaye kuilaumu Serikali kutaka ichukue hatua.

Aidha, Rais Kikwete alisema Serikali inatambua mchango wa kanisa la Anglikana katika maendeleo ya nchi na itaendelea kutoa ushirikiano katika kuimarisha huduma zinazotolewa na kanisa hilo, ikiwemo huduma za afya na elimu.

Kwa upande wake, Askofu Chimeledya aliitaka Serikali kuongeza juhudi kwa kupambana na ufisadi, rushwa, madawa ya kulevya na mauaji ya vikongwe na walemavu wa ngozi, kwa kuwa vinalidhalilisha taifa.

Askofu huyo alisema pia Kanisa Anglikana linaiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kwa wale wanaotumia udini kufanya vitendo vya chuki na hivyo kuondoa umoja na mshikamano ulioasisiwa kwa miaka mingi.

“Sisi viongozi wa dini tutaendelea kuhubiri amani, umoja na utulivu, ila tunaiomba Serikali kuchukua hatua madhubuti kwa redio, magazeti na cd ambazo zinaeneza chuki za kidini.

“Serikali pia ichukue hatua kwa wale wanaoeneza uvumi kwamba Wakristo wanapendelewa, kwamba mfumo wa Serikali ni wa Kikristo, tusiwe na chuki, kama huduma za jamii kama afya na elimu zinazotolewa na taasisi za Kikristo zinahudumia Watanzania wote bila kujali dini wala kabila la mtu,” alisema.

Askofu huyo pia alizungumzia hali ya kanisa kwa kusema kwamba siyo nzuri kwa sasa, kutokana na migogoro mingi, hivyo ni vyema kumuomba Roho Mtakatifu ili aweze kufanya kanisa kuwa moja.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template