RAIA nane wakiwemo wanne wenye asili ya Kiarabu kutoka nchini Saudi Arabia na
Watanzania wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Arusha kwa tuhuma za
kuhusika na mlipuko wa bomu lililotokea katika uzinduzi wa Kanisa la Mtakatifu
Joseph, Parokia ya Olasiti mkoani Arusha, juzi.
Habari ambazo Tanzania Daima imezipata kutoka jeshi la polisi mkoani Arusha,
zinadai kati ya Watanznaia wanaoshikiliwa mmoja anatoka Babati ambaye ndiye
anayedhaniwa kurusha bomu hilo.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, raia hao wa Saudi Arabia walikamatwa
juzi mchana wakiwa njiani kuelekea Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Inadhaniwa watu hao walikuwa wakitoroka hapa nchini, lakini walishindwa
kufikia azma yao hiyo kutokana na msako mkali wa Jeshi la Polisi ulioanzishwa
baada ya kutokea kwa tukio hilo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, watuhumiwa hao walihojiwa jana mchana katika
ofisi za makao makuu ya polisi mkoani Arusha ambapo hata hivyo Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi, hakuwa tayari kueleza kile walichokisema.
Wakati huohuo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alikwenda mkoani Arusha katika
eneo la tukio akazungumza waumini kanisani na baadaye kwenda kwa balozi wa
Vatikan hapa nchini na mwakilishi wa Papa Francis, Askofu Fransisco Padilla.
Waziri Mkuu leo anatarajia kwenda katika Hospitali za KCMC na Mount Meru
kuwajulia hali wagonjwa waliojeruhiwa na mlipuko huo ulioutikisa mji wa
Arusha.
Wakati huohuo viongozi wa dini, serikali na vyama vya siasa nchini wameungana
kutaka utulivu na uvumilivu katika kipindi hiki ambacho taifa limo katika hali
ya sintofahamu kutokana na tukio la kigaidi la kushambuliwa waumini wa Kanisa
Katoliki, mjini Arusha, juzi.
Waumini hao walifikwa na mkasa huo juzi majira ya saa 4 asubuhi wakiwa katika
Misa ya Jubilee ya miaka 50 ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Rais wa Baraza la Maakofu Tanzania (TEC)
Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Sheikh wa BAKWATA wa mkoa wa Dar es
Salaam, Alhad Mussa Salim, wamewataka Wakristo na Waislam kuwa watulivu na
kuviacha vyombo vya usalama vifanye kazi ya kuchunguza wahusika wa tukio
hilo.
Wakati viongozi wa dini nchini wakionyesha mshikamano huo, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete jana alikatiza ziara yake ya kiserikali
nchini Kuwait na kurejea nyumbani kuungana na viongozi wenzake wa serikali na
dini kushughulikia tukio hilo.
Akitoa taarifa ya Rais Kikwete kukatiza ziara yake, Mkurugenzi wa Mawasiliano
Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa Rais Kikwete alitarajiwa kurejea nyumbani
leo, lakini alilazimika kukatiza ziara hiyo na kurejea nyumbani mara moja kuwa
karibu na wafiwa pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la
kigaidi.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake mjini
Iringa, Askofu Ngalalekumtwa, alisema kwamba ni utamaduni wa Wakristo wote
duniani kuzidisha sala na maombi wakati wanaposhambuliwa na kudhuriwa ili atoe
jibu kwa wanaohusika na vitendo hivyo.
“Kasi ya sala iendelee ili Mungu wetu wa Amani ajenge fikira za upendo na
haki katika mioyo yetu, sala ndiyo silaha yetu pekee na tunaamini Mungu
atatujibu kwa kuwafichua watu waliohusika na vitendo hivi vya kihalifu,” alisema
askofu Ngalalekumtwa.
Aliwataka waumini kuwa watulivu na kutokata tamaa kuomba kwani Mungu ndiye
mwenye jibu na atatoa majibu kadiri atakavyo kwa wale wote wanaowatesa wenzao
kwa sababu zao binafsi.
“Tulieni na kufanya tafakuri kisha mwambieni Mungu hayo yote ayafanyie kazi
kwa uweza wake. Sisi binadamu tunategemea nguvu kutoka kwake,” alisema na
kuongeza: “Waliopoteza maisha wapokee Rehema ya Mungu na waliojeruhiwa
wafarijiwe na uwezo wa Mungu,” alisema.
Alisema kuwa wakati huu ni wa kutafakari na kumkabidhi Mungu yale yote
yanayowasumbua wanadamu na kuongeza nguvu ya sala ili majibu ya Mungu yapatikane
kwao.
Kwa upande wake Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salim amewataka
Watanzania kuwa watulivu na wavumilivu na kujizuia kutuhumiana au kutoa matamshi
yenye kuchochea mgawanyiko wa kidini baina yao, wakati huu vyombo vya usalama
vinapoendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kigaidi.
“Kwanza kabisa nawapa pole waliofiwa na ndugu zao katika shambulizi hilo, na
ninawatakia kheri ya kupona haraka wale wote waliojeruhiwa. Pili ninawaomba
Watanzania kuwa watulivu na wavumilivu wakati huu vyombo vya usalama vinapofanya
uchunguzi wa wahusika wa shambulizi hilo, tusianze kunyosheana vidole na
kutoleana kauli za kufarakana kidini,” alisema Salim.
Naye mwenyekiti wa taasisi ya Imam Bukhary ya jijini Dar es Salaam, Sheikh
Khalifa Khamis, ameitaka serikali kuyadhibiti haraka makundi ya Waislam
yanayoeneza chuki na kuhamasisha kuua watu, kuchoma nyumba za ibada za dini
zingine ili kulinda na kudumisha utulivu na amani ya nchi.
Alitaka viongozi wa dini, hasa wa Kiislam kutokubali dini yao kutumika na
vikundi hivyo kama anuani ya kufanya maovu na kwamba wapaze sauti na kukana
maovu hayo kwamba hayahusiani na imani ya Kiislam.
Alisema kuwa ni wakati muafaka sasa kwa masheikh kutumia njia zinazowezekana
ili kuwafahamisha Waislam katika misikiti yao, mikutano mbalimbali ya hadhara na
katika shughuli za kidini kwamba ni lazima kufuata mfumo wa Uislam unaokataza
maovu.
Alisisitiza kuwa mafundisho ya dini, yanasisitiza amani, upendo baina ya watu
wote, na ndio utamaduni ulioenziwa tangu zamani, hivyo si sahihi kutumia mgongo
wa dini kufanya mambo yanayokwenda kinyume na sheria.
Sheikh Khalifa alinaani kitendo cha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia
yaliyofanywa na magaidi mjini Arusha na kuongeza kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji
wa haki za binadamu.
Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Freeman Mbowe ametuma salaam za pole na rambirambi kwa waumini wa
Kanisa Katoliki nchini na Watanzania wote kwa ujumla kutokana na shambulizi hilo
lililotokea katika Kanisa la Olasiti, jijini Arusha, lililosababisha vifo na
majeruhi, huku wengine wakipatwa na mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, kwa vyombo
vya habari, Mbowe alitoa salaam hizo alipozungumza kwa njia ya simu na Katibu wa
Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Antony Makundi, juzi Jumapili jioni,
baada ya kupata taarifa za tukio hilo la kigaidi.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) aliwataka
Watanzania wote kuwa watulivu wakati huu, ambapo serikali kupitia vyombo vya
dola inafanya uchunguzi wa tukio hilo.
Aliitaka serikali kuchunguza na kutoa taarifa haraka kuhusu tukio hilo na
matukio mengine yote ya namna hiyo ili kuwapatia Watanzania matumaini ya
kuendelea kuishi kwa utulivu na amani katika nchi yao.
Baadhi ya wakazi wa kawaida wa jiji la Dar es Salaam wamelitupia lawama Jeshi
la Polisi nchini kuwa ndio chanzo cha mashambulizi ya Arusha kutokana kushindwa
kuwakamata baadhi ya watu tangu kuibuka kwa vitenodo hivyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tanzania Daima jijni Dar es Salaam jana,
kuhusu tukio la kushambuliwa watu waliokuwa kanisani juzi, wakazi hao walisema
kama jeshi hilo halitakuwa makini huenda vitendo hivyo vikazidi kuendelea
nchini.
Walisema kuna matukio ya kushambuliwa viongozi wa kidini, mgogoro kuhusu
kuchinja na kutekwa na kuteswa kwa baadhi ya watu kutokana na mazingira ya kazi
zao hata hivyo, hadi leo hakuna aliyekwishakamatwa kuhusiana na matukio
hayo.
Mmoja wa wakazi hao Mushi Shayo, alisema huu si wakati wa kunyoosheana vidole
bali wanaopaswa kulaumiwa ni jeshi la polisi kutokana na kushindwa kwao
kuwabaini watu hao wanaoleta chokochoko za kigaidi.
Alisema kutowataja watu waliohusika na matukio mbalimbali ndiko kunakochangia
baadhi ya watu hao wabaya kuendelea kufanya vitendo vyao hivyo.
Naye mwanaharakati, Amos Joseph, alisema umefika wakati kwa Watanzania kuacha
kushabikia mambo bila kujua matokeo yake kwani wataipeleka nchi pabaya.
Alisema kuna watu hivi sasa wamekwishayapa muelekeo mashambulizi hayo kuwa
yalifanywa na watu wa upande fulani kitendo ambacho kinazidi kujenga uhusiano
mbaya katika jamii.
Tayari jeshi la polisi nchini limesema kuwa linawashikilia watu wanane kwa
tuhuma za kuhusika na mlipuko huo, wanne kati yao ni raia wa Saudi Arabia na
wengine ni Watanzania.
Mlipuko huo ulitokea katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Parokia ya
Olasiti Arusha mjini, juzi Jumapili, na kusababisha vifo vya watu wawili na
kujeruhi 70.
SOURCE:TANZANIA DAIMA.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !