RAIS ATEUWA NAIBU MAKATIBU WAKUU WAPYA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ameteua Naibu Makatibu Wakuu tisa (9) wa Wizara mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne tarehe 20 Julai, 2010 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Kiongozi, Bwana Phillemon Luhanjo inaonyesha kuwa uteuzi wa Naibu Makatibu Wakuu hao unaanzia tarehe 15 Julai, 2010 na wataapishwa rasmi siku ya Alhamisi tarehe 29 Julai, 2010 saa 4.00 asubuhi.
Taarifa hiyo imewataja walioteuliwa kuwa ni pamoja na Bwana Ngosi C.X. Mwihava, Kamishna Msaidizi (Nishati Mbadala) katika Wizara ya Nishati na Madini kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya Bwana Luhanjo, Rais Kikwete amewateua Balozi Herbert E. Mrango ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kanda katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Miundombinu; Balozi Rajab Gamaha ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Uganda kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na Bwana Mbogo Futakamba, Mkurugenzi wa Umwagiliaji na Ufundi ambaye sasa anakuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Katika Uteuzi huo, Rais Kikwete pia amewateua Dk. Yohana L. Budeba ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, na Bibi Maria H. Bilia ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Aidha, Rais Kikwete amewateua Bibi Nuru H.M. Mlao ambaye kwa sasa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii; Bwana Hussein A. Katanga ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, na Bwana Job D. Masima ambaye ni Mkurugenzi katika Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
20 Julai, 2010
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !