Mtihani darasa la saba 1998:
Manispaa Moro yaagiza ipewe majina ya wanafunzi
Wakatoliki
- Wazazi Waislamu wapigwa na bumbuwazi
- Walimu wakuu watuhumiwa
Na Rajab Rajab, Morogoro
WASI WASI mkubwa umeanza kuwaingia wazazi Waislamu wa mjini hapa kufuatia
kupatikana kwa barua kutoka ofisi ya Elimu Manispaa inayowaagiza walimu wakuu
wote wa shule za msingi kupeleka majina ya wanafunzi Wakatoliki wa darasa la
saba wa mwaka huu.
Mapema juzi baadhi ya Waislamu walionekana kupigwa na bumbuwazi
baada ya kupata taarifa hizo na baadhi yao wakiwa wameiona nakala ya barua
hiyo.
Gazeti hili lilifanikiwa kuipata nakala ya barua hiyo ambayo imetiwa saini na
mtu aitwaye E.P. Mpessa kwa niaba ya Afisa Eimu wa Manispaa ya Morogoro.
Katika barua hiyo yenye kumbukumbu namba E.10/MMC-1/183 iliyoandikwa Juni 9
mwaka huu, inawataka walimu wakuu wote wa shule za msingi Manispaa ya Morogoro
kutuma majina ya wanafunzi Wakatoliki darasa la saba hadi kufikia Juni 12,
1998.
Barua hiyo fupi haikufafanua kiundani majina hayo ni ya nini jambo ambalo
limewafanya Waislamu wa hapa kuanza kuwatilia mashaka walimu wakuu wa shule hizo
kuwa wanafahamu suala hilo kiundani zaidi ndio maana Mwandishi hakulazimika
kufafanua.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya Waislamu wamedai kuwa vitu vya namna
hiyo ndivyo vinavyowafanya waumini wa dini ya Kiislamu kuituhumu serikali kuwa
inawapendelea Wakristo katika nyanja zote na hususan katika elimu.
"Hali hii na mikakati kama hii viongozi wetu wa Kiislamu walio serikalini
hawajui na wakipewa taarifa kama hii huwa hawaifanyii kazi badala yake
wanawarushia Waislamu kashfa kwa kuwaambia hawana dira", alisema kwa uchungu
muumini mmoja wa eneo la Kingo Bwana Ally Seifu.
Naye Bw. Athman Salim wa Mafiga amesema "hata watoto wetu wasipochaguliwa
kujiunga na shule za sekondari za serikali mwakani tutaamini kuwa imetokana na
njama hizi."
Kufuatia kupatikana waraka huo baadhi ya waumini wametishia kulipeleka suala
hili mbele ya sheria (mahakamani) kwa madai kuwa linahatarisha hali ya baadaye
ya vijana wao kimasomo.
Aidha baadhi ya waumini hao wa Kiislamu wameiomba serikali kutopuuzia hali
hii na kwamba ufanyike uchunguzi wa kina kwa kuunda tume huru vinginevyo huenda
kukatokea mgawanyiko miongoni mwa raia wake.
Mitihani ya Darasa la Saba inatarajiwa kufanyika nchi nzima mwezi Septemba
mwaka huu.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !