Mbio za urais zaingia kanisani
- Lowassa tayari ashika mwaliko wa 2013
- Sitta, Membe wapigana vikumbio
- Mbowe: Mimi hasitaki urais
MAKADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaotajwa kutaka urais mwaka 2015, wameanza mbio katika nyumba za ibada, MwanaHALISI imebaini.
Waliotajwa hadi sasa ni Edward Lowassa, Samwel Sitta na Bernard Membe.
Hata hivyo Sitta alinukuliwa wiki iliyopita akiwa jimboni kwake Urambo, Tabora akisema anachukizwa na wanaomhusisha na mbio za urais mwaka 2015.
Sitta ni mbunge wa Urambo Mashariki aliyekuwa spika wa bunge la Muungano na sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Membe, ni mbunge wa Mtama na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Edward Lowassa, mbunge wa Monduli tayari ametajwa kukaribishwa kwenye harambee ya ujenzi wa ofisi za Dayosisi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), mwaka kesho (2013).
Kwa mujibu wa mtoa habari, Lowassa ataongoza harambee ya kwanza Jumapili ijayo, 22 Januari. Hii inahusu ujenzi wa Dayosisi ya Shinyanga.
Mtoa taarifa anasema tayari jina la waziri mkuu wa zamani aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya kutoa mkataba wa kuzalisha umeme kwa njia ya upendeleo, lipo katika ratiba ya kuongoza mikusanyiko ya kuchangisha fedha.
Taarifa zinasema harambee nyingine itafanyika Julai mwaka huu na gazeti hili limethibitishiwa kuwa Lowassa ndiye atakayekuwa mgeni rasmi wa kuongoza harambee hiyo.
Kiongozi wa kanisa la KKKT jimbo kuu la Mwanza, Askofu Andrea Ngulle ameliambia MwanaHALISI kuwa wamemwalika Lowassa kuongoza harambee ya Jumapili, lakini akakana kufahamu ugeni wa Lowassa kwa harambee ya Julai.
Lowassa taarifa zinasema tayari anatembea na mwaliko wa kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa kanisa moja kwenye eneo la Kanda ya Ziwa Viktoria iliyopangwa kufanyika kati ya Septemba na Oktoba mwaka kesho.
Aidha, baadhi ya wapambe wake wamenukuliwa na mtoa taarifa wetu wakisema “tumejipanga ili kuhakikisha baada ya kukamilisha ziara za makanisani, aanze ziara za aina hiyo misikitini.”
Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja siku tatu baada ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu kuwataja Lowassa, Sitta na Membe kuwa ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliojipanga kuwania urais mwaka 2015.
Akiongea katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Nyalandu alisema pamoja na kwamba wote watatu ni marafiki zake, lakini hakuna hata mmoja ambaye ameanza kumuunga mkono.
“Nimeamua kueleza haya ili kuweka rekodi sawasawa baada ya baadhi ya wapambe wao kuanza kunigombanisha. Nimesema na narudia tena kusema, sihusiki na hata mmoja miongoni mwao,” alisema Nyalandu katika mahojiano na gazeti hili juzi Jumatatu.
Nyalandu alikuwa akijibu swali juu ya kilichosababisha kuchukua uamuzi wa kuwaanika anaoita “marafiki” zake na vita vya urais.
Nyalandu ambaye ni mbunge wa Singida Kaskazini, amesema yeye ni rafiki mkubwa wa viongozi wote hao watatu na ni haki yake kuhusishwa nao; lakini hahusiki na harakati za yeyote kwa dhamira ya kutafuta urais.
Amesema yeye ana kazi moja tu kwa sasa: Kumtumikia Rais Jakaya Kikwete kwa wadhifa aliomteua wa naibu waziri.
Nyalandu amewataja viongozi hao wakati wenyewe hawajawahi kutangaza kutafuta urais ingawa baadhi yao wamekuwa wakionekana kwenye harakati zinazoelekea huko.
Mara kadhaa Lowassa na Sitta wamehudhuria hafla zilizoandaliwa na makanisa kwa ajili ya kuchangisha fedha za ujenzi wa miradi ya kanisa.
Hata hivyo, Sitta amesema anachokifanya ni kutumikia tu umma kwa sababu hana nia ya kuwania urais mwaka 2015.
Sitta amenukuliwa akisema urais ni jambo linalokuja lenyewe kwa watu waadilifu, hivyo hakuna haja kwa watu kila siku kufanya harakati za urais.
“Urais unakuja wenyewe kwa watu walio waadilifu. Nachukizwa na watu ambao kila siku wamekuwa na mawazo ya urais na kuacha mambo ya msingi ya kutumikia wananchi,” amefafanua Sitta.
Amesema wapo wanaojaribu hata kutengeneza uongo kwamba amekuwa akienda makinisani na misikitini kwa ajili ya kutaka urais; lakini anasisitiza, “Hawa ni walewale mafisadi wanaoeneza ajenda zao za ovyo kila siku.”
Sitta alifafanua kwamba suala la yeye kusaidia shughuli au kujumuika katika Kanisa au Msikiti ni jambo la kawaida na hakuanza kulifanya leo wala jana.
Amesema wapo wanaojaribu kujenga taswira kwa umma kuwa kujumuika kwake katika baadhi ya shughuli za makanisa au misikiti ni sehemu ya mbinu za kusaka urais kitu alichosema ni upotoshaji kwa kuwa hakuanza leo kujumuika na wana dini.
Wakati hayo yakiendelea, Freeman Mbowe, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amenukuliwa na mtoa taarifa wetu akisema, “Mimi sitaki urais.”
Mbowe ambaye aliwahi kugombea urais kwenye uchaguzi wa mwaka 2005, anadaiwa kusema dhamira yake kwa sasa ni kujenga chama chake ili kiweze kushinda urais.
“Nakuambia kaka, mwenyekiti hataki kabisa urais. Haya mambo yanayoandikwa kwenye vyombo vya habari, ni propaganda inayopikwa na mmoja wa viongozi ambaye anatafuta umaarufu kwa maslahi yake binafsi,” alisema mbunge mmoja wa chama hicho kwa sharti la kutotajwa gazetini.
Amesema, “Nimekutana mara kadhaa na mwenyekiti (Mbowe) na amenihakikishia kuwa hana nia wala hafikirii kugombea nafasi hii ya urais. Amesema kazi yake sasa ni kwenda mikoani kujenga chama kwa kufungua matawi na mashina. Basi.”
Gazeti limepata ushahidi wa kutosha kwamba habari za urais zinazohusisha na mbio za urais ndani ya chama hicho, zinapikwa na kiongozi huyo (jina tunalo); mpango huo unasukwa kwa ustadi mkubwa na mmoja wa wahariri nchini.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !