- Kitoloho
Headlines News :
Home » »

Written By Msamaa on Tuesday, May 7, 2013 | 10:20 PM

Viongozi wa dini wakataa mihadhara.

Dar es Salaam.

 

Viongozi wa Serikali, Bunge na wale wa dini Mkoa wa Dar es Salaam, wameshauri kuzuiwa kwa mihadhara ya wazi ya dini na kupendekeza ifanyike ndani ya nyumba za ibada.
Ushauri huo umekuja huku kukiwa na matukio kadhaa yanayotishia amani kwa misingi ya dini kama kushambuliwa na kuuawa kwa viongozi wa dini, kuchomwa moto wa nyumba za ibada na mgogoro wa kuchinja.
Akifungua kongamano la dini lililoandaliwa na uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam jana, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha alisema mihadhara inachangia tatizo la udini ambalo limejitokeza katika siku za karibuni kauli ambayo iliungwa mkono na viongozi wa madhehebu ya Kikristo na Kiislamu.
Wakati viongozi hao wakisema hayo, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini akichangia mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi bungeni jana, alilitaka Jeshi la Polisi kuzuia utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara ambayo alidai inachochea vurugu za kidini.

Nahodha
Nahodha alisema mihadhara mingi imekuwa ikiendana na kashfa za wafuasi wa dini moja dhidi ya nyingine... “Lugha za kashfa zinazotolewa katika mihadhara hii husababisha waumini wa dini nyingine kuhamaki na kulipiza kisasi. Inafaa mambo haya yaendeshwe ndani ya nyumba za ibada.”
Aliwataka viongozi wa dini kuchunga ndimi zao kwa sababu zinaweza kuwa chachu ya migongano ya kidini.
“Inasikitisha kuona kuwa tumetimiza miaka 50 kama taifa lakini watu hawajajifunza madhara ya vita vinavyotokana na ubaguzi wa kidini na kikabila kama ilivyowahi kutokea katika nchi za Rwanda, Lebanon na Ivory Coast,” alisema Nahodha, ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar kuanzia mwaka 2000-2010.
Alionya kuwa Serikali haitasita kutumia nguvu za dola dhidi ya wote wanaotaka kuchochea mitafaruku ya kidini.

Viongozi wa dini

Akichangia katika kongamano hilo ambalo liliandaliwa maalumu kukuza mshikamano miongoni mwa wafuasi wa dini mbalimbali nchini, Askofu Mkuu wa Kanisa la Afrika Inland Church (AIC), Dayosisi ya Pwani, Charles Salala alisema mihadhara si jambo baya, bali watu wanaotumia nafasi hiyo kutoa lugha za kashfa dhidi ya waumini wengine.
Alisema kutokana hali hiyo, waumini wa dini zote wanapaswa kuheshimiana na kuishi kwa pamoja ili kuondoa tofauti zinazoweza kuhatarisha amani.
Askofu Salala alitolea mfano suala la kuchinja akisema katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru, hilo halikuwa tatizo lakini sasa hali imekuwa tofauti.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Musa Salum alisema Waislamu na Wakristo ni ndugu na hawapaswi kuwa na tofauti ambazo zinaweza kuhatarisha amani.
“Sisi ni wamoja, kwa nini tugombane, tunapaswa kushirikiana pamoja ili kuondoa tofauti zilizopo ambazo zinaweza kuhatarisha amani,” alisema Sheikh Salum, ambaye aliunga mkono haja ya mihadhara kufanyika kwenye nyumba za ibada.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema waumini watakaobainika kwenda kinyume katika mihadhara, watachukuliwa hatua za kisheria.
“Mihadhara haikatazwi, watu wanatakiwa kufuata sheria na taratibu za nchi, ikiwa tutawabaini wanakwenda kinyume na kuhatarisha amani tutawakamata,” alisema.

Selasini

Mbunge huyo wa Rombo aliilaumu Serikali kwa kuwaachia watu kufanya mihadhara kwa miaka 20. Alionya kuwa ikiwa mikutano hiyo isipozuiliwa, itaongeza vurugu za kidini nchini.
“Hata wanaozungumza lugha za uchochezi kwenye mikutano ya hadhara washtakiwe, kwa sababu tunamtafuta mchawi wakati sisi wenyewe ndiyo tunaochochea kuigawa nchi,” alisema Selasini na kushangiliwa na wabunge wenzake.
CHANZO:MWANANCHI.08/05/2013.

Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template