SERIKALI imefuta matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2012 na kuagiza yaandaliwe upya.
Uamuzi huo ulitangazwa jana bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi.
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Lukuvi alisema uamuzi huo wa serikali umetokana na mapendekezo ya Tume ya Waziri Mkuu iliyoundwa kuchunguza chanzo cha matokeo ya kidato cha nne mwaka jana kuporomoka kwa kiwango cha kutisha.
Waziri Lukuvi alisema kutokana na umuhimu wa mapendekezo hayo, Baraza la Mawaziri limeamua kwamba utekelezaji wa mapendekezo hayo uanze mara moja.
Kwa mujibu wa Lukuvi, uchunguzi wa awali wa tume hiyo ulibaini kuwa pamoja na wanafunzi hao kuwa katika mazingira yanayofanana na wenzao wa miaka ya nyuma, ufaulu wao umeshuka kutokana na mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo kwa mwaka 2012.
“Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyopita na mfumo huo ndio uliosababisha matokeo mabaya,” alisema.
Akifafanua tofauti ya mfumo wa 2011 na 2012, Waziri Lukuvi alisema mwaka 2011 Baraza la Mitihani la Taifa lilikuwa linachakata alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika kutegemea hali ya ufaulu wa mwanafunzi ambao ni National Mean Difference (NMD).
Utaratibu huu ulitokana na tofauti ya wastani wa kitaifa wa alama za maendeleo kutoka alama za maendeleo endelevu (Continued Assessiment - CA) za watahiniwa wote na wastani wa kitaifa wa ufaulu wa mitihani ya mwisho kwa somo husika.
Alisema chini ya mfumo huo, kila mtahiniwa aliongezewa NMD iliyokokotolewa katika alama za mtihani wa mwisho ili kupata alama itakayotumika kupata daraja la ufaulu.
“Kimsingi, kila somo lilikuwa na NMD yake kulingana na CA zilivyo kwa mwaka husika,” alisema Lukuvi.
Lakini mwaka 2012, Waziri Lukuvi alisema Baraza la Mitihani la Taifa lilitumia mfumo mpya wa kuwa na viwango maalumu vya kutunuku (Fixed Grade Rangers).
Alisema tume hiyo ya uchunguzi iliyoongozwa na Profesa Sifuni Mchome ilibaini kuwa mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri, lakini haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya kutumika.
Kutokana na kasoro hiyo, Lukuvi alisema tume hiyo imependekeza matokeo yote ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yafutwe na yaandaliwe upya kwa kutumia utaratibu wa mwaka 2011.
Pia imependekeza uwiano (standardisation) ufanyike ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi walizoziweka katika kusoma kwenye mazingira na hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa taifa kuongeza idadi ya shule na wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea.
Tume hiyo imelitaka Baraza la mitihani kutambua kuwa pamoja na sheria ya kuanzishwa kwake, inawaruhusu kufanya marekebisho ya mchakato wa mitihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya mitihani lazima yahusishe wadau wote wanaohusika na mitaala, ufundishaji na mitihani.
“Wakati tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Baraza la Taifa la Mitihani wa kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya mitihani uliotumika mwaka 2012 usitishwe.
“Badala yake utumike utaratibu wa mwaka 2011 kwa kidato cha nne na cha sita kwa mitihani yote ukiwemo utaratibu wa uwiano na kutoa matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, mchakato wa Mfumo wa Tuzo wa Taifa (National Qualifications Framework) na Mfumo wa kutahiniwa/kutathmini maendeleo ya mwanafunzi katika masomo yake (National Assessment Framework) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.
Akizungumzia utekelezaji wa maazimio hayo, Waziri Lukuvi alisema Baraza la Mawaziri limeamua kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo uanze mara moja.
Alisema Baraza la Mawaziri limeitaka tume hiyo kuendelea kukamilisha taarifa yake vizuri kwa kuhusisha wadau mbalimbali ili kupata maoni zaidi na ushauri wao juu ya mambo mbalimbali yaliyobainika wakati wa uchunguzi kabla ya kuikamilisha na kuitoa kwa matumizi ya umma.
Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012 yalionesha kuwa ufaulu umeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni.
Matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni, yalionesha kwamba kati ya wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu.
Katika idadi hii, wanafunzi waliofaulu katika daraja la kwanza hadi la tatu ni 23,520, sawa na asilimia 6.4 na daraja la nne ni 103,327, sawa na asilimia 28.1.
Watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 ya wanafunzi wote, waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012, walipata daraja sifuri.
Source:TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !