MABADILIKO YA KWELI YANATOKANA NA UAMUZI MGUMU.
MUSTAKABALI wa nchi yenye amani na mafanikio ya kiuchumi miongoni mwa
jamii; yapo mikononi mwa wananchi wenyewe na sio wanasiasa. Wanasiasa ni
wananchi miongoni mwa wananchi ambao hufuata miongozo ya chama cha siasa.
Miongozo hiyo inaposhindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa hulka na mifumo
inayofuata chaguo la mikondo ya kimataifa, huufumbia macho utu kwa kulazimisha
wananchi kufikiri vile wanavyotaka wao wafikiri. Kazi kubwa ya chama cha siasa
ni kushika hatamu katika nchi. Ukisikiliza hoja za baadhi ya wachambuzi kuhusu
mwelekeo wa nchi, mmeng’enyo wa kifikra na matokeo ya chambuzi zao,
yanahalalisha matukio kwa hoja nyepesi kwamba; yanayotukia hayawezi kuepukika
kwa kuwa hata nchi zilizoendelea zilipitia katika aina ya matukio yanayoipitia
nchi yetu.
Kwa chambuzi hizo, wananchi wanaambiwa kutii mabadiliko kwa njia yoyote,
iwe ya kufa na kumwaga damu, basi mathalani ni matazamio ya kisiasa wanastahili
kupata stahili ya kile wanachotarajia kukipata kupitia siasa za wakati. Hata
kama mwananchi atapitiwa na kitu chenye ncha kali tumboni, usoni, mdomoni,
kifuani anatakiwa kutii mapito, kwa kuwa kwa kufanya hivyo itamsadia kufikia
kule walikofikia wengine katika nchi zilizoendelea. Chambuzi hizi ukizipasua na
kuona “utumbo” uliomo ndani yake kama umekaa sawasawa, majibu ya wakati
kutokana na vipimo vya wakati utabaini kwamba wale waliokuwa wakitazamiwa
kielimu kuwa viongozi wenye fikra mpya, bado wana matatizo ya urithi wa
kufikiri.
Matatizo ya urithi wa kufikiri ni janga ambalo pia limejielekeza katika
siasa za nchi kupitia mifumo ya urithi wa kimataifa. Hisia na mihemuko ya
kisiasa inatatiza mwelekeo sahihi wa nchi. Ni wananchi pekee ndio wenye uwezo
wa kuiweka nchi katika hali ya amani na mafanikio kwa njia ya kujitambua pale
walipo na wapi wanataka kwenda; na wanatumia njia ipi kufikia matazamio yenye
afya endelevu. Viongozi wa siasa waliotoa ahadi mwaka 2010, wameanza kuandaa
ulaghai wa mwaka 2015 dhidi ya wananchi wangali bado hawajatekeleza ahadi
walizoahidi.
Mbaya zaidi, Bunge letu limepewa majina kama vile bunge la mipasho,
bunge la komedi, bunge la kampeni, nani anajali maisha yako? Je, inatosha
kusema bunge letu la mipasho? Je, inatosha kushabikia siasa zisizo na shibe kwa
wananchi? Je, nini matokeo ya ushabiki wa kisiasa? Kwa ufupi, wanasiasa wanahujumu
akili zetu kupitia njia za hatari ilihali wao wakibaki salama na familia zao.
NIONAVYO MIMI; wananchi lazima watimize wajibu wao kwa kufanya kazi na kukataa
viongozi wenye malengo binafsi. Malengo ya kisiasa yaliyojikita katika kuwagawa
Watanzania kwa itikadi za kidini na maeneo ni lazima yazikwe kupitia fikra mpya
za wananchi. Lazima wananchi wapaze sauti dhidi ya matumizi mabaya ya kodi zao
kwa kuwalipa wabunge wachafuzi wa lugha, badala ya kujadili mambo ya msingi,
vinginevyo tungemtumia babu wa kifimbo cheza awachape bakora. Wananchi watambue
na kujitambua kwamba wao ndio taa ya nchi.
NIONAVYO MIMI; siasa za nchi zinapoteza mwelekeo na kutoleta tumaini
lolote kwa wananchi, hivyo ni wajibu wa wananchi kutambua hilo linahitaji fikra
zao mpya badala ya zile za urithi kwamba ni kipindi cha mpito. Haya ni maneno
ya wavivu wa kufikiria ambao fikra zao zimeganda na kukosa mwelekeo unaofaa
kuzuia hatari itokanayo na mapito. Hisia na mihemko ya uchu wa madaraka ni
ajenda ya siasa ambazo bila wananchi kujitambua na kuzidhibiti, siku si nyingi
tutashuhudia hali ya hatari ikijitokeza miongoni mwa jamii zisizokuwa na hatia.
Lazima wananchi waache upofu walionao wa kufikiri upande mmoja wa kubeba vipofu
wenzao wasioona kwamba hawahusiki katika mambo ya maendeleo ya wananchi. Tuache
kumung’unya maneno.
SOURCE:www.kiongozi.co.tz/
Posted by Mhariri Kiongozi May 2, 2013.
Posted by Mhariri Kiongozi May 2, 2013.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !