SIKU iliyopangwa kuwa ya kupokea wanajeshi wetu mashujaa waliorejea nchini
kutoka Uganda mwaka 1979, sherehe kubwa katika Kata ya Malangali ziliandaliwa
katika viwanja vya Shule ya Sekondari Malangali.
Ilikuwa siku ya furaha. Wanajeshi walisimulia walivyomtia adabu nduli Idd
Amini Dada, walieleza walivyolisambaratisha Jeshi la Uganda lililokuwa na vifaa
vingi na zaidi umakini wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na umahiri wa
kitengo cha upelelezi.
Msemaji Mkuu wa wanajeshi wale alijinasibu kuwa Tanzania ni ya tatu duniani
baada ya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na Mosad ya Israel, kwa uwezo wa
kuchunguza mbinu za maadui na kuzivuruga.
Alisema hata uwezo wa kuchunguza matukio maovu yaliyotekelezwa na adui
Tanzania ina uwezo mkubwa.
Masimulizi mengine ya kivita hayakuwa yanasikika kutokana na wananchi
kushangilia kupita kiasi na kina mama walipiga vigelegele kusifu majeshi
yetu.
Hiyo ilikuwa Malangali tu, kwingineko nchini kulikuwa na hadithi za
kusisimua, kutia moyo. Ya Dar es Salaam sikuyajua, mimi nilikuwa Malangali.
Leo nikiwa kwenye chumba cha habari najiuliza kimetokea nini hadi maadui wa
amani yetu wanaingia nchini, wanapanga nyumba zetu, wanatengeneza vilipuzi na
kufika kwenye eneo na kuhujumu bila wanajeshi wetu kujua?
Leo nikiwa ndani ya chumba cha habari, najiuliza kimetokea kitu gani hadi
Jeshi la Polisi limebaki kutegemea msaada wa Shirika la Upelelezi la Marekani
(FBI) kwa matukio ambayo hata raia wanayajua?
Nachelea kuunga mkono hoja ya wapinzani kwamba Jeshi la Polisi livunjwe,
lakini ukweli limekuwa mzigo, limesahau au limeacha majukumu yake, limebaki kuwa
kitengo maalumu cha propaganda na mkono wa mateso wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Bila FBI, polisi wetu hawawezi kuchunguza tukio lolote na wakifanya watatoka
na matokeo ya ajabu. Walichunguza tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Steven
Ulimboka wakatoka na mtuhumiwa ambaye Dk. Ulimboka anasema siye.
Mpaka leo wameshindwa kumkamata aliyemtesa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri,
Absalom Kibanda; na mbaya zaidi polisi wameshindwa kuwanasa polisi saba
waliomzingira mwandishi wa habari wa Kituo cha Channel 10, Daudi Mwangosi,
wakamsulubu na hatimaye kumlipua kwa bomu la machozi.
Uwezo wa polisi wetu umedorora tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990. Kipindi
hicho polisi hawakubaini njama zilizopangwa na Waislamu wenye msimamo mkali
kwenda kuvamia na kuvunja mabucha ya nguruwe katika eneo la Manzese, Dar es
Salaam. Mwanazuoni mmoja maarufu wa Kiislamu alitajwa kuhusika.
Aidha, tukio la Agosti 7, 1998 la kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani nchini
liliwaumbua polisi wetu; hawakujua hata pa kuanzia.
Watu 11 walikufa na 85 walijeruhiwa. Polisi wakapata mahali pa kujitetea
baada ya muda kama huo siku ileile Ubalozi wa Marekani nchini Kenya kulipuliwa
na kusababisha vifo vya watu 212 na majeruhi karibu ya 4,000.
Hapo ndipo tulishuhudia polisi wetu wakihamanika, simu na ‘radio call’
mikononi lakini walikuwa wanazuga tu. Makachero wa FBI walipokuja ndio walibaini
magaidi hao kwamba waliingia nchini Juni 1998.
FBI ndio waligundua kwamba waliolipua ni kikundi cha Egyptian Islamic Jihad
cha nchini Misri chenye fungamano na al-Qaeda ambacho kilisema kitazungumza na
Marekani kwa lugha inayoijua vema.
FBI walibaini kwamba mawakala waliingia nchini wakapanga nyumba moja eneo la
Ilala na walikuwa wanatumia gari aina ya Suzuki Samurai. Ukweli makachero
walipata taarifa nyingi na gereji iliyotumika katika kuandaa boksi.
Makachero hao walifanikiwa kumnasa Ahmed Ghailani wa Zanzibar na kueleza kuwa
ni wakala wa kikundi hicho chenye uhusiano na kikundi cha al-Qaeda kilichokuwa
kinaongozwa na Osama bin Laden.
Badala ya kutumia mafunzo waliyopata kwa ajili ya kuihami nchi, polisi wetu
wakayatumia mafunzo hayo kupambana na kuvikomoa vyama vya upinzani. Akili zao
zikawa kwenye siasa – wapewe ukuu wa wilaya, ukuu wa mkoa na ubunge.
Polisi Zanzibar wakawanasa na kuwabambikia kesi ya uhaini Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na baadaye Juma Duni Haji na
wenzake 18 wakabambikiwa kesi kama hiyo wakafungwa.
Mwaka 2001 polisi waliwapiga wafuasi wa CUF waliokuwa wanaandamana kwa amani
eti intelejensia yao ilibaini kwamba walitaka kuteka kituo cha polisi na
kuchukua silaha. Wafuasi wapatao 27 walichinjwa kwa risasi.
Kwa vile, serikali ilishapitisha sheria ya ugaidi, mwaka 2005 walijifungia
wakachora mchoro wa ugaidi na namna nzuri ya kuwabambikia CUF ili kuinusuru
CCM.
Hapo aliibuka aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omari Mahita,
akatangaza kuwa CUF wameingiza majambia kwa ajili ya kuanzisha machafuko baada
ya Uchaguzi Mkuu mwaka ule.
Japokuwa tuhuma zile ni za kigaidi, Mahita aliishia hapo, hakumkamata mtu
wala kumshtaki yeyote kuhusiana na madai hayo.
Mahita hakueleza waliyakamata kwenye meli, ndege na idadi na hakueleza
viongozi waliohusika na hatua alizochukua. Kwa hofu watu waliipigia tena CCM
ikapeta.
Katika matukio makubwa ya ugaidi kama huu wa kulipuliwa Kanisa Katoliki la
Parokia ya Mt. Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha, intelejensia ya polisi iko
mahututi.
Wakati Machi 13, 2013 polisi waliitangazia dunia kumkamata kwa tuhuma za
kupanga ugaidi, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare,
makanisa zaidi ya 30 yamelipuliwa nchini, baadhi ya viongozi wa dini kuuawa na
wengine kujeruhiwa vibaya, polisi hawajui.
Kinachosikitisha ni kwamba, polisi si tu wameshindwa kubaini njama mapema,
kama wanavyofanya kwa wanasiasa, bali pia hawana uwezo hata wa kupeleleza.
Mifano ni kama ifuatavyo. Shambulio hilo lililofanywa na mtu asiyejulikana
Jumapili ya Mei 5, 2013, wakati wa uzinduzi wa kanisa hilo la Parokia ya Mt.
Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Arusha, polisi hawakujua licha ya kwamba baadhi
walikuwa eneo la tukio.
Jambo zuri waliohusika kurusha bomu na kupanga njama hizo wamekamatwa kwa
msaada wa FBI na Interpol. FBI ndio wamesaidia hata Zanzibar kama itakavyoelezwa
hapa chini.
Desemba 9, 2011, Kanisa la Silom, Kianga Mkoa wa Kusini Unguja lilibomolewa
na watu wanaosadikiwa ni Waislamu wenye msimamo mkali na Kanisa la Pefa la
Mtufaani, Mwera, Wilaya ya Magharibi, Unguja lilichomwa moto.
Oktoba 12, 2012 Waislamu wenye msimamo mkali walivamia na kuchoma moto
makanisa matano huko Mbagala Wilaya ya Temeke. Madai yao ni kupinga kitendo cha
mtoto mmoja wa Kikristo kukojolea juzuu katika mabishano baina ya mtoto huyo na
mwenzake wa Kiislamu.
Novemba 6, 2012 Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga,
kutokana na msimamo wake juu ya uthabiti wa Muungano wa sasa, alimwagiwa
tindikali na mtu asiyejulikana wakati akifanya mazoezi huko karibu na nyumbani
kwake Mwanakwerekwe.
Desemba 26, 2012 Padri Ambrose Mkenda wa Parokia ya Mpendae, Zanzibar
alipigwa risasi na watu wasiojulikana nje ya nyumba yake jioni wakati akitoka
kanisani.
Februari 11, 2013 Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God,
Mathayo Kachila aliuawa katika vurugu za kugombea uhalali wa kuchinja kati ya
Wakristo na Waislamu huko Geita.
Siku sita baadaye yaani Februari 17, 2013 Padri Evarist Mushi aliuawa kwa
risasi alipokuwa akielekea Kanisa la Mt. Theresia, Mtoni Zanzibar.
Matukio haya yote, ukiacha la kuharibiwa makanisa Mbagala, kuuawa kwa Padri
Mushi na ugomvi wa Geita, polisi hawajawakamata wahusika katika matukio hayo
mengine.
Vilevile, polisi walifanikiwa kuwanasa walioharibu makanisa ya Mbagala baada
ya kudai ni wahuni tu si Waislamu wenye msimamo mkali. Lakini aliyemuua Padri
Mushi alikamatwa na makachero wa FBI.
Ziko wapi tambo kwamba Tanzania ni ya tatu kwa uwezo wa kuchunguza matukio ya
kihaini na kigaidi baada ya CIA na Mosad?
Ziko wapi tambo kwamba Tanzania inashika nafasi ya tatu kupeleleza matukio
baada ya FBI? Je, ni kutokana na siasa kuathiri jeshi hilo au kukwepa matukio
yenye fungamano na dini? Hapa ndipo lilipo tatizo.
Bila FBI polisi hawawezi kunasa magaidi wa ukweli isipokuwa waliopangwa kwa
ushirikiano na CCM. Mfano anayetajwa kuwa ndiye alipanga njama za kumteka na
kumpeleka eneo la mateso Dk. Ulimboka ni Ofisa Usalama wa Taifa lakini polisi
wamemkamata raia wa Kenya.
Kwa vile, katika kipindi kifupi FBI wametusaidia kuwanasa watu 10 waliohusika
na mlipuko wa Arusha, na wametusaidia kumkamata mshukiwa wa mauaji ya Padri
Mushi, wananchi tunaomba FBI ichunguze pia kupata ukweli wa watu waliomteka,
kumtesa Dk. Ulimboka, waliomtesa Kibanda, waliowaua Mwangosi na Issa Ngumba wa
Redio Kwizera.
Ikiwa nchi hii itaingia katika machafuko watu wa kwanza kubeba lawama
watakuwa polisi.
Miaka ya 1960 polisi ndio waligundua njama za mapinduzi yaliyowahusisha pia
Bibi Titi na wengineo.
Polisi weledi na wazalendo waligundua njama za mapinduzi mwaka 1983 na
matukio mengine.
Lakini polisi wa leo licha ya kujengewa uwezo wanaua raia na kunyang’anya
mali kama kesi ya Abdallah Zombe na wanatesa kama Dk. Ulimboka na Kibanda.
CHANZO: TANZANIA DAIMA.
|
Ndugu yangu jina lako tu linadhihirisha wazi kwamba wewe ni bwamdogo kiasi kwamba kuna mambo unahitaji kusaidiwa ili uwe uelewa wa kutosha. Kukusaidia tu Waislamu tangu uhuru huu upatikane waliandamwa na mpaka leo wanaendelea kuandamwa na moja katika sababu ya kuandamwa ni kwamba wametupwa nje katika viunga vya uongozi licha ya jitihada kubwa waliyoifanya kupigania uhuru huku Nyerere akiwa kama mualikwa kusindikiza jahazi la watu na shughuli zao. Kwa hiyo shutma hizo ulizonazo sisi hazitushangazi dhidi ya Waislamu kwani ndani ya nchi hii wamehalalishiwa majina yote mabaya na pia ni halali nguvu za dola kuwaangukia kwani nchi inaendeshwa kwa mfumo kristo. Sasa kusikia jambo fulani wamesingiziwa wao au kuitwa Wahuni wanapodi haki zao si jambo geni mana wao wanalelewa na mama wa kambo asiyewapenda hata kidogo "Tanzania" Ila hujui kwanini ripoti hazitolewi hadharani baada ya uchunguzi na kukusaidia tu ni kwamba wale ambao hudhaniwa kwamba ndio waliotenda, baada ya uchunguzi huthibitika si wahusika kwani "NGUVU YA DHANA HUZIMWA NA YAKINI"
ReplyDelete