Chanzo: Tanzania Daima 14/05/2013.
MIILI ya watu wawili akiwemo mtoto wa mchungaji wa kanisa la Tanzania
Assemblies of God (TAG) lililo kwenye kitongoji cha Rehani, kata ya Tutuo,
wilayani Sikonge, Tabora imeopolewa kwenye dimbwi la maji katika mazingira ya
kutatanisha.
Mtoto wa mchungaji huyo aliyetambuliwa ni Pascal Yasin (27) na Utukufu
Stefano Bugore (16) ambao ni wanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari ya
Tutuo.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu vifo hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi
mkoa wa Tabora, Edward Bukombe alikiri kupokea taarifa hiyo kutoka kwa watu
waliotembelea eneo hilo.
Alisema marehemu hao hawakuwa na jeraha lolote katika miili yao ila mmoja
alikuwa akitoka damu puani huku akibainisha kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha
kwamba marehemu walikuwa wakiogelea kwenye dimbwi hilo.
“Marehemu mmoja alikuwa na nguo ya ndani tu huku mwenzake akiwa na suruali
bila shati, hivyo inawezekana walishindwa kuogelea wakazama… kwa sababu hawana
alama yoyote ile katika miili yao,” alisema kaimu kamanda huyo.
Kwa mujibu wa Bukombe Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Sikonge
amebainisha kuwa marehemu walizama baada ya kushindwa kuogelea hivyo wakanywa
maji mengi. Aidha uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Awali mchungaji wa kanisa hilo wilayani Sikonge, Michael Namba, alisema upo
uwezekano watu hao wameuawa kwa vile mchungaji wa kanisa la Tutuo hutumiwa
ujumbe wa vitisho.
“Meseji zote za vitisho tunazo na tumetoa taarifa kwa polisi wa hapa Sikonge
ili ziwasaidie katika uchunguzi wao, kwani hili lilipangwa… na vitisho hivyo
vinaendelea,” alisema mchungaji Michael Namba.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !