RAIS KIKWETE AMPONGEZA MHASHAMU GERVAS JOHN NYAISONGA ASKOFU MPYA JIMBO KATOLIKI DODOMA.
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA IBADA YA KUMWEKA WAKFU ASKOFU MTEULE GERVAS JOHN NYAISONGA WA JIMBO KATOLIKI DODOMA, TAREHE 19 MACHI, 2011, DODOMA
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
Mhashamu Askofu Mkuu, Jude Thaddaeus Ruwaichi,
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania;
Mhashamu Baba Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Dodoma,
Gervas John Nyaisonga;
Mzee wetu Benjamin William Mkapa,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Waheshimiwa Mawaziri;
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, Eng. James Nsekela,
Viongozi wa Dini Mbalimbali Mliohudhuria;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana:
Tumsifu Yesu Kristo!
Shukrani na Pongezi
Awali ya yote napenda kuungana nanyi kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kujumuika hapa siku hii ya leo. Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Jimbo Katoliki Dodoma kwa heshima kubwa mliyonipa ya kunishirikisha katika siku ya leo ya kihistoria ya kuwekwa wakfu na kusimikwa Mhashamu Baba Askofu Gervas John Nyaisonga kuwa mchungaji mkuu wa Wanakondoo wa Jimbo Katoliki Dodoma. Nimeipokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa na moyo wa upendo. Ni kielelezo tosha cha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Serikali na Kanisa Katoliki.
Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga;
Kwa niaba yangu na kwa niaba ya wananchi wote wa Tanzania na Serikali, nakupongeza sana kwa kuteuliwa kwako na leo hii kwa kuwekwa wakfu na kuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki wa Jimbo la Dodoma. Uteuzi wako kushika nafasi hii nyeti ni kielelezo cha imani kubwa aliyonayo Baba Mtakatifu Benedicto wa Kumi na Sita (XVI) kwako. Imani hiyo ya Baba Mtakatifu ndiyo imani waliyonayo kwako waumini wa Jimbo la Dodoma. Naambiwa waliithibitisha imani hiyo tangu walipokupokea mpakani Gairo mpaka ulipofika hapa Dodoma. Umati huu mkubwa uliojaa hapa leo unadhihirisha tena ukweli huo. Hata sisi wakazi wengine wa Dodoma ambao si waumini wa Kanisa Katoliki tunaungana nao kwa matumaini hayo.
Matarajio Yetu kwa Mhashamu Askofu Nyaisonga
Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga,
Uwanazuoni wako, uadilifu wako, uaminifu wako na utiifu wako kwa kiapo chako cha Upadre, na kwa Kanisa lako, ndivyo vilivyowapa waamini wa Jimbo lako matumaini makubwa kwa uongozi wako wa kiroho. Aidha, sifa yako ya kupenda maendeleo inaleta matumaini siyo tu kwa waamini hata kwa sisi ambao si wafuasi wa dini yako, pia tuna matumaini hayo.
Matumaini hayo makubwa ni jambo jema sana lakini pia ni deni na changamoto kubwa sana kwako. Unao mtihani mkubwa kwani inaelekea watu wana matumaini makubwa mno pengine hata kupita kiasi. Bahati nzuri wewe bado kijana kwa umri na hivyo kwa rehema za Mwenyezi Mungu, unao muda mrefu mbele wa kuwatumikia waamini wa jimbo hili. Bila ya shaka, kwa sifa kubwa uliyonayo ya kuwa kiongozi makini, mpangaji mzuri wa mipango na mtekelezaji mahiri, matumaini yetu yatatimia. Sote tunakuombea kwa Mola akuwezeshe. Bila ya shaka Bwana hatakutupa mkono bali atakuongoza na kukusaidia.
Ushirikiano wa Serikali na Madhehebu ya Dini
Mhashamu Baba Askofu Gervas John Nyaisonga;
Napenda kuitumia nafasi hii kukuhakikishia ushirikiano wangu binafsi na ule wa wenzangu wote Serikalini katika utekelezaji wa majukumu yako hasa pale ambapo mchango wa Serikali utakapohitajika. Serikali yetu ina historia ya miaka mingi ya ushirikiano na madhehebu ya dini zote pamoja na Kanisa Katoliki. Nilishasema mara kadhaa siku za nyuma na leo napenda kurudia tena kusema kuwa tutafanya kila tuwezalo kuudumisha na kuuendeleza uhusiano na ushirikiano wetu huu.
Nasema hayo kwa sababu ya manufaa ya dhahiri yanayotokana na ushirikiano wetu huu. Serikali inanufaika na Kanisa linanufaika lakini kubwa zaidi taifa linanufaika na wananchi wake wanafaidika. Madhehebu ya dini nchini yamekuwa yanashirikiana vyema na Serikali hasa katika kuwapatia wananchi huduma muhimu kama vile elimu, afya, maji n.k. Kanisa Katoliki ni miongoni mwa madhehebu ya dini yaliyoko mstari wa mbele katika mambo haya. Watanzania wengi wa dini zote na hata wale ambao bado hawajaamua kujiunga na upande wowote wananufaika na huduma zinazotolewa na Kanisa hili.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Wahashamu Maaskofu, Wageni Waalikwa;
Kwa kutambua na kuthamini mchango muhimu wa madhehebu ya dini katika kuongezea nguvu jitihada za Serikali za kuwahudumia wananchi wake, ndiyo maana Serikalini tumekuwa tunasaidia madhehebu ya dini kwa namna mbalimbali kufanikisha shughuli zao hizo. Ukiacha misamaha ya kodi kwa jumla inayotolewa kwa madhehebu ya dini, kwa upande wa elimu hivi sasa, Serikali inatoa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vyote vya elimu ya juu nchini bila ya kubagua. Kabla ya hapo mikopo ilikuwa inatolewa kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu vya Serikali tu.
Kwa upande wa huduma ya afya Serikali imekuwa inatoa ruzuku kwa hospitali na zahanati za mashirika ya dini ambazo tuna Makubaliano ya Huduma (Service Agreement). Chini ya utaratibu huo, kwa mfano, Serikali inatoa ruzuku ya vitanda katika hospitali na kulipia mishahara baadhi ya madaktari na wauguzi. Tumeiongeza ruzuku ya vitanda kutoka shilingi 7,500/= kwa mwaka, kwa kitanda mwaka 2004 hadi shilingi 50,000/= kwa kitanda hivi sasa. Mwaka 2009 kulikuwa na vitanda 5,600 katika hospitali 60 zilizokuwa zinanufaika na mpango huu. Hivi sasa vimeongezeka.
Kwa sababu hiyo mwaka 2009 Serikali imechangia shilingi 45 bilioni, mwaka 2010 tukaongeza zikafikia shilingi 54 bilioni na mwaka huu wa 2010/11 tumetenga shilingi 61.9 bilioni kama ruzuku kwa hospitali za mashirika ya dini mbalimbali nchini ambazo zinatoa huduma kama hospitali teule za wilaya na rufaa. Hospitali ya Bugando, KCMC na CCBRT zimenufaika sana chini ya utaratibu huu. Aidha, Serikali inatoa ruzuku ya shilingi 30,000/= kwa kila mwanafunzi kwa mwaka katika vyuo vya afya vya mashirika ya dini. Serikali, pia imekuwa inashikiza wakufunzi wake katika vyuo hivyo kwa gharama yake. Kwa ajili hiyo, mwaka 2009/10 Serikali ilitumia shilingi 107,580,000.
Mhashamu Askofu Gervas John Nyaisonga;
Nimeyasema haya kukuhakikishia kuwa kwa mipango ya maendeleo ya kuendeleza huduma muhimu katika Jimbo lako tegemea ushirikiano wa Serikali usiokuwa na shaka. Ni utaratibu tuliojiwekea, tutauenzi na kuuendeleza. Natambua katika Jimbo la Dodoma kuna mipango ya kujenga Sekondari ya St. Peter Claver kule Ihumwa na siku za usoni mnao mpango wa kujenga Chuo Kikuu katika eneo hilo. Nafahamu pia kwamba Hospitali ya Miyuji iliyo chini ya Shirika la Masista wa Mt. Gema inategemewa kupandishwa hadhi na kuwa hospitali teule ya Wilaya ya Dodoma. Miradi yote hiyo itanufaika chini ya utaratibu wetu wa ushirikiano tulionao. Natoa pongezi nyingi kwa kazi nzuri mnayoifanya. Nawaomba muendelee kufanya hivyo na Serikali itaendelea kuwaunga mkono.
Ninalo ombi kuhusu elimu kwa madhehebu ya dini na wawekezaji binafsi nchini kwamba waelekeza uwekezaji wao katika kuongeza nafasi za kidato cha tano na sita. Kwa sababu ya kuwepo sekondari za kata mahitaji ya nafasi hizo yanazidi kuongezeka na Serikali haitatosheleza yote. Naomba tusaidiane. Mwaka huu tumechukua vijana 36,826 kuingia kidato cha tano, lakini wapo wengi wenye sifa na hawakubahatika. Hivyo, basi ninawasihi muwekeze katika shule za kidato cha tano ili kuweza kutoa nafasi zaidi kwa vijana wetu.
Maadili Mema Katika Taifa
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
Wahashamu Maaskofu, Waheshimiwa Viongozi wa Dini;
Napenda kutumia nafasi hii pia kuwaomba viongozi wa dini muendelee kufanya kazi ya kulilea taifa letu kiroho na kimaadili. Natambua ugumu wa kazi hiyo katika dunia ya leo ya utandawazi ambapo maadili mema ya jamii pamoja na mila na desturi zetu havionekani kupewa thamani kubwa. Matokeo yake ni matendo ya utovu wa maadili mema kuenea karibu kila mahali. Bahati mbaya na inasikitisha zaidi kuona kwmba baadhi yetu wanayaona mambo hayo maovu yanayomchukiza Mungu ni ya kawaida au ndiyo mambo ya kisasa au kwenda na wakati. Siku hizi si ajabu kumkuta mtoto mdogo akimtukana mtu mzima au watu wazima wakitoleana lugha chafu, kuvaa mavazi yasiyositiri maungo, au kufanya mambo ambayo kimsingi yanamchukiza Mwenyezi Mungu. Naambiwa huko kwenye mitandao ndiyo usiseme, kunahitaji moyo wa ujasiri kuhimili mambo machafu yaliyomo na lugha inayotumika. Vitendo na matukio ya uhalifu kama vile wizi, rushwa, matumizi ya dawa za kulevya, ubakaji, mauaji n.k. yanazidi kuongezeka siku hadi siku.
Waheshimiwa Viongozi wa Dini na Wageni Waalikwa;
Mimi na wenzangu Serikalini tunatambua wajibu wetu wa kupambana na uhalifu na utovu wa maadili kwa mujibu wa sheria. Kwa kutumia vyombo vya dola tunajitahidi sana na bado tunaendelea na juhudi hizo. Pamoja na hayo, jamii na hasa viongozi wa kiroho mnayo nafasi maalum ya kuweza kusaidia katika jitihada hizi. Ninyi ni viongozi mnaoheshimika sana na waamini wenu na jamii kwa jumla na kauli zenu zinabeba uzito wa aina yake. Nawaomba muitumie fursa hiyo adimu na adhimu kuhubiri na kuhimiza waamini wenu na watu wote kwa jumla wawe wacha Mungu wa dhati na kuona thamani ya kutenda mema na kuacha kutenda mambo mabaya, ili hatua kwa hatua tulirejeshe taifa katika maadili mema.
Jambo lingine ninalowaomba viongozi wa dini muendelee kuiombea nchi yetu ipate mvua za kutosha, mabwawa yajae, umeme upatikane na nchi iwe na chakula cha kutosha. Kadhalika msichoke kuiombea nchi yetu amani na upendo miongoni mwa wananchi wake. Jambo kubwa la kusisitiza hapa ni kuwataka watu wapendane, washirikiane na kamwe wasibaguane kwa rangi, kabila, dini, jinsia, maeneo wanayotoka au itikadi za kisiasa. Haya ni miongoni mwa mambo ya tunu ambayo Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere alituachia Watanzania. Ndiyo siri ya amani na utulivu wa nchi yetu. Hatuna budi kuyaenzi na kuyaendeleza.
Nawaomba viongozi wa dini muwe mstari wa mbele kuwakumbusha waamini wenu, wananchi na hata sisi wanasiasa kuzingatia tunu hizi. Msichelee kumkemea mtu yeyote anayetaka kupandikiza chuki na kuwagawa Watanzania kwa tofauti zao. Tukishindwa kwa hili, hakika amani na utulivu vitatuponyoka na hilo likitokea haitabiriki lini tutaipata tena. Na siye tutakuwa kama walivyo wenzetu ambao sote tunawajua walipoichezea amani iliwaponyoka na hadi sasa wanajuta. Hivi sasa wanahangaika kuitafuta amani au kurejesha utulivu waliokuwa nao kabla ya machafuko.
Uvumulivu Miongoni mwa Waamini
Ndugu Zangu Viongozi wa Dini;
Rai yangu ya mwisho kwa viongozi wa dini ni kuendelea kuhimiza Watanzania wote pamoja na sisi wanasiasa kuvumiliana kwa tofauti zetu za rangi, kabila, dini na itikadi za kisiasa. Hizi ni tofauti ambazo hatuna budi kutambua kuwa zipo, zilikuwepo na zitaendelea kuwepo. Hatuna namna ya kuziondosha zikafutika kabisa. Hivyo basi, tuzikubali na kujifunza kuishi nazo. Kuvumiliana ndilo jambo la msingi na ndiyo uwe mwongozo wetu sote.
Lazima tutambue kuwa mambo ya msingi yanayotuunganisha ni ubinadamu wetu na uraia wetu wa Tanzania. Kwa sababu hizo, kila mmoja wetu anazo haki sawa na kwamba hakuna mtu aliyemzidi mwenzake. Hata mimi Rais sijamzidi mwananchi wa kawaida kwa haki zake za binadamu na kama raia wa Tanzania.
Nawaomba viongozi wa dini na wanasiasa tuendelee kuhubiri na kuhimiza kuvumiliana, kuheshimiana na kushirikiana miongoni mwa Watanzania kwa misingi ya ubinadamu wetu na uraia wetu licha ya tofauti zetu. Nasisitiza tuendelee kufanya hivyo kwa sababu tumekuwa tunafanya hivyo kwa mafanikio makubwa tangu Uhuru mpaka sasa. Ndiyo maana nchi yetu ina amani na utulivu. Kwa nini tushindwe leo miaka 50 baadae? Hatuwezi kusema kuwa tumechoka amani. Hatuwezi kujifanya au kuonekana hatujui athari za kuchukiana na kubaguana. Kwa vyo vyote vile amani na utulivu vitatoweka na tukifika hapo tutakuwa tumepata hasara kubwa sana. Tutakosa muda wa kujiletea maendeleo, tutakosa muda wa kwenda makanisani au miskitini na badala yake watu watakuwa wanahangaika kunusuru maisha yao dhidi ya jirani yao aliyegeuka adui.
Mimi binafsi na Serikali ninayoiongoza tutafanya kila lililo ndani ya uwezo wetu kuhakikisha kwamba Tanzania haifiki hapo. Hatuna budi tushirikiane kuepusha balaa hilo. Naomba tusaidiane kujenga jamii yenye kutambua kuwa haki na wajibu havitengemani. Tujenge jamii ya watu wanaopendana wenyewe kwa wenyewe, wanaoshirikiana, wanaoshikamana na wanaopenda amani na utulivu wa nchi yao.
Mwisho
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo,
Wahashamu Maaskofu na Wageni Waalikwa;
Baada ya kusema maneno mengi hayo, naomba kurudia tena kuwashukuru kwa kunishirikisha katika sherehe hii muhimu na adhimu. Tuendelee kushirikiana na kusaidiana kwa maslahi ya taifa letu na watu wake. Naomba nirudie tena kutoa pongezi zangu kwa Mhashamu Askofu Gervas John Nyaisonga kwa kuteuliwa kwako, kuwekwa wakfu na kutawazwa leo kuwa Askofu wa Jimbo la Dodoma. Sote tumuombee kwa Mwenyezi Mungu aweze kumudu majukumu yake, tumpe ushirikiano ili aweze kuifanya vema kazi aliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu ya kuwahudumia waamini wa Jimbo Katoliki Dodoma. Ninawatakieni nyote furaha na fanaka tele katika kusherehekea siku hii tukufu.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !