TANU
Jimbo la Tanga, 1956
ILIKUWA ni huko Tanga
tu katika historia ya Tanganyika kuwa dhana mpya katika siasa zaidi ya ule
ubwana wa Wazungu uliongezwa katika uhusiano baina ya Waafrika na Waarabu.
Dhana hii iliongezwa ndani ya mfumo wa siasa za Tanganyika ili kuwakinza
Waafrika katika siasa. Hiki kilikuwa kitu ambacho Waafrika walikuwa
hawajapambana nacho. Kwa zaidi ya karne moja walikuwa wamezoea ubwana wa
Wazungu. Jimbo la Tanga lilibarikiwa na kuwa na Waafrika walioelimika sana.
Waafrika hawa walikuwa kutoka kabila la Wabondei. UMCA ilikuwa imehama
kutoka Zanzibar kwenda Magila katika Jimbo la Tanga mwaka 1875. Ukristo
ulianzishwa na kustawi katika nchi ya Wabondei, na vivyo hivyo nafasi za
elimu kwa watoto wa Wabondei. Katika lile wimbi la kuwania nafasi za elimu,
watoto wengi wa Kiislamu walibatizwa. Ni jambo la kawaida miongoni mwa
Wabondei kukuta majina kama Peter Saidi au John Ramadhani. Huu ni ukumbusho
wa damu ya Kiislam katika Wabondei. Wabondei wengi walikwenda Makerere College
na siasa za kizalendo zilipoanza baada ya Vita Kuu ya Pili, Wabondei
walikuwa wamejaa katika utumishi wa serikali ya kikoloni. Gurudumu la
historia ya Tanganyika likizungushwa na baadhi ya Wabondei, maarufu
miongoni mwao wakiwa watu kama Martin Kayamba aliyejikomba sana kwa
wakoloni, George Magembe mtu ambae huku alikuwa hayuko wala kule hayuko,
hujui kama yupo na wazalendo au na wakoloni, Stephen Mhando; mzalendo
mwenye msimamo mkali na na mdogo wake Peter.
Wabondei walikuwa ndiyo
walimu, makarani, wakalimani mahakamani na maofisa wa ustawi wa jamii
katika serikali ya kikoloni. Hili lilikuwa tabaka maalum la Waafrika,
waliosomeshwa na wamishonari kuitumikia serikali ya kikoloni na katika
kufanya hivyo kulitumikia Kanisa na Ukristo, uhusiano ambao ulikuwa wenye
manufaa kwa pande zote mbili zilizokuwa zikishirikiana. Ilikuwa vigumu sana
kwa Wabondei kutokana na upendeleo huo wasifikirie kwamba wana uhusiano
maalum na Kanisa na serikali ya kikoloni. Hawa Waafrika wasomi kutoka shule
za misheni na Makerere walikuwa watiifu kwa taasisi mbili zanye nguvu
nchini, yaani serikali ya kikoloni na Kanisa. Kwa ajili hii basi, ilibakia
kwa Wadigo Waislam wasiokuwa na elimu kama elimu ilivyokuwa ikiitikadiwa,
kuunda TANU na kuongoza harakati za kudai uhuru.
Wamishionari waligundua
kuwa Wadigo walikuwa wagumu sana kubatizwa na kuingizwa kwenye Ukristo kwa
sababu ya imani yao thabiti katika Uislam. Kwa hiyo Wadigo hadi hii leo
wamebakia kuwa kabila la Waislam. Baada ya kuukuta Uislamu umeimarika vyema
katika pwani ya Tanga, wamishonari kwa kukataa kuhasimiana na Waislam,
walianzisha misheni zao ndani zaidi mbali na pwani sehemu inayojulikana
kama Misheni ya Magila. Hapa UMCA ilianzisha shule na hospitali. Wadigo
walishikilia imani yao ya Kiislamu na wakabakia nyuma katika elimu kwa
sababu ya kukataa kwao Ukristo. Kwa jili hii wakajinyima nafasi za kazi za
madaraka katika seriklai ya kikoloni. Huku kuwapanga watu kwa tabaka
kulikuwa na athari katika kuanzisha upinzani dhidi ya ukoloni kwa kuwa
waliofadhiliwa na Kanisa walishindwa kupinga wakoloni kwa kuwa ukoloni na
Ukristo walikuwa wamoja.
African Association
huko Tanga ilikosa umoja baina ya wale walioitwa 'wasio na elimu na
wasiojua kusoma' na wale wasomi ambao kutoka kwao wote hawa chama cha siasa
kingeweza kuundwa. Waafrika wasomi, Wabondei waliunda vikundi vyao peke yao
vya wasomi kutokana na juhudi za ofisa mmoja wa kikoloni. Vyama hivi
vikijulikana kama Discussion Groups 167 yaani, vikundi
vya majadiliano, vilitarajiwa kutojihusisha na kisiasa na vilitiwa nguvu na
serikali kuhimiza mijadala na kusoma vitabu. Katika muda wote wa uhai wa
vikundi hivyo hawa wasomi wa Makerere walikuwa chini ya usimamizi wa afisa
Mzungu.
African Association
huko Tanga ilitawaliwa na watu wa mchanganyiko wa damu ya Kiarabu na
Kiafrika. Hawa walikuwa watu wenye elimu ndogo. Kundi hili halikuwa na
mkabala mzuri na Wabondei wengi wao wakiwa Wakristo wenye elimu. Kundi hili
lililokuwa na damu ya Kiarabu lilijiona bora kwa daraja kuliko Waafrika
weusi. 168 Kama hivi vikundi viwili muhimu vingeweza kuzikusanya
pamoja nguvu tofauti zao, vingeweza kuunda umoja wa siasa wenye uwezo
mkubwa sana kama ile kamati ndogo ya siasa ya TAA iliyoundwa huko Dar es
Salaam. Muungano huu ungeweza kuongoza harakati za kudai uhuru huko na
halikadhalika ungeweza kupata mafanikio makubwa kwa kuwashirikisha wananchi
katika kudai haki zao. Lakini kama ilivyokuwa, hizi kambi mbili zilikuwa
hasimu; kila upande ukijitenga mbali na umma; wengine walijiona bora kwa
sababu ya rangi ya ngozi yao na wengine walijiona bora kwa sababu ya elimu
yao.
Gavana Edward Twining
alipounda Constitutional Development Committee mwaka 1949, na kukaribisha
maoni na mapendekezo kutoka kwa raia, TAA Tanga ilijikuta haina uwezo wa
kuandika waraka. Uongozi wa Waarabu katika African Association haukuwa na
elimu, maarifa au ujuzi uliotakiwa kutayarisha na kuandika waraka kwa
serikali. Wasomi wa Makerere katika vile vikundi vya majadiliano
waliinyakua fursa hiyo na kuandika waraka ambao uliwakilishwa kwa Gavana
Twining.169 Pamoja na ukweli kuwa waraka ule uliandikwa na
Waafrika wenye elimu kubwa kwa wakati ule, kwa hakika waraka ulikuwa na
upungufu ukilinganisha na ule ulioandikwa na kamati ndogo ya siasa ya TAA,
Dar es Salaam.170
Mwaka mmoja baadae,
katika mwaka 1951 ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulipozuru Tanganyika, kile
kikundi cha majadiliano, ingawa si wawakilishi wa wananchi kikifanya kazi
yake nje ya TAA, kiliwasilisha waraka kwa ujumbe huo kikionyesha kuwa wao
wanawakilisha maoni ya Waafrika. Hili lilizusha mzozo baina ya wasomi wa Makerere
na ule uongozi wa Waarabu katika TAA.171 Haya makundi mawili
yalijikuta hayana kusudio au muelekeo wenye maana, kidogo kidogo
yalisahaulika. Kule Tanga mara chache watu waliihusisha ofisi ya TAA na
siasa. Ofisi ya TAA inakumbukwa na kuhusishwa na mahakama ambako Kadhi,
Sheikh Ali bin Hemed alihukumu jamii ya Waislam kwa kutumia sharia.
Lakini Tanga iliibuka
mwaka 1955 na kukabiliana na serikali ya kikoloni kupitia juhudi binafsi za
kikundi cha wafanyabiashara wadogo wadogo katika soko la Ngamiani. Kikundi
hiki kiliongozwa na kijana Peter Mhando, katibu wa zamani wa kile kikundi
cha majadiliano cha wasomi wa Kibondei. Akikiongoza kikundi hiki ambacho
kilikuwa na Waislam, alikuwa baharia mstaafu, Hamis Heri Ayemba. Hamis Heri
alikuwa Mmanyema kutoka kabila la Wakusu wa Belgian Congo. Peter Mhando
alikuwa akifanya kazi kama mhandisi katia Noran Industries- wanunuzi wa
nazi na watengenezaji sabuni pale Tanga. Hamisi Heri alikuwa na umri wa
katikati na katika ujana wake alikuwa baharia na alipata kusafiri chombo
kimoja na Abeid Amani Karume, ambae baadae alikuja kuwa rais wa Zanzibar.
Baada ya Vita Kuu ya Pili, Hamisi Heri alirudi kwao Tanga ili aanze
biashara. Heri alikuwa mtu aliyejikuza na kujielimisha mwenyewe; na alikuwa
amesafiri sana. Hamisi Heri alizungumza vizuri sana Kiingereza na Kiarabu.
Katika miaka yake ya mwanzo katika biashara, alikuwa dalali. Heri
aliwashangaza wateja wake kwa uhodari wake wa lugha mbali mbali, akinadi
bei kwa Kihindi au Kiarabu, kutegemea utaifa wa watu waliokuwepo pale mnadani.
Harakati za kudai uhuru
zilipoanza Heri alikuwa ametajirika na mmoja wa Waafrika wenye kuheshimiwa
sana mjini Tanga. Mhando alipochoshwa na kile kikundi cha majadiliano,
alijiunga na Hamisi Heri na kikundi cha Waislam wa pale mjni ambao walikuwa
wakijitahidi sana kuunda tawi la TANU. Wakati huo mwanasiasa mwenye uzoefu
mkubwa kuliko wote mjini Tanga alikuwa Mwalimu Kihere.172 Lakini
siasa za mapambano baina ya ule uongozi wa TAA chini ya Waarabu na kikundi
cha majadiliano zilimzuia kutoa mchango wowote wa maana. Mwalimu Kihere
alikuwa amehudhuria mikutano kadhaa ya African Association tangu mwaka
1946. Wakati wa uongozi wa Abdulwahid Sykes alikuwa amedumisha uhusiano
mkubwa sana baina yake yeye mwenyewe binafsi, Abdulwahid na Dossa Aziz. Hii
ilifanya vilevile adumishe mawasiliano ya karibu sana na makao makuu ya
TAA. Lakini kwa sababu ya mizozo katika siasa hapo Tanga, ule mkutano mkuu
wa kuasisiwa TANU uliofanyika Dar es Salaam mwaka wa 1954 ulipita bila ya
Tanga kupeleka mjumbe.
Kile kikundi cha wafanyabiashara
wadogo wadogo katika soko la Ngamiani kiliitisha mkutano katika Ukumbi wa
Tangamano tarehe 5 Septemba, 1955. Waliohudhuria mkutano huo walikuwa Hamis
Heri, Peter Mhando, Mohamed Kajembe,173 Tuwa Abdallah, Dhili
Mgunya, Abdallah Rashid Sembe, Victor Mkello,174 Mohamed Sadik,
Hassan, Peter Ramadhani Jembe na Ali Mohamed. Peter Ramadhani tayari
alikuwa mwanachama wa TANU huko Arusha na alikaribishwa mkutanoni ili
waasisi wa TANU wanufaike kutokana na uzoefu wake. Wasomi wa Makerere,
uongozi wa TAA chini ya Waarabu na Mwalimu Kihere hawakuwepo kwenye mkutano
huu muhimu. Mkutano ulifunguliwa na Hamis Heri saa tisa adhuhuri na
ulifungwa saa mbili baadae kwa uamuzi kuwa mkutano mwingine wa kuchagua
viongozi wa chama ufanyike tarehe 23 Oktoba. Mkutano uliamua vilevile kuwa
juhudi zifanyike kupata waanachama wengi iwezekanavyo. Kiasi kidogo cha
fedha kilikusanywa na Harir Omari Siagi alipewa aende makao makuu ya TANU,
Dar es Salaam kununua kadi sabini za TANU.
Tarehe 23 Oktoba,
wanachama wa mwanzo wa TANU huko Tanga walikutana kuchagua uongozi wao
chama. Hamisi Heri alichaguliwa kuwa mwenyekiti na Peter Mhando katibu.
Jumla ya watu arobaini na tano walihudhuria mkutano huo na wakapewa kadi za
TANU. Mwalimu Kihere alihudhuria mkutano ule lakini hakuchaguliwa katika
nafasi yoyote ya uongozi. Kamati ya wanachama iliundwa kutokana na wale
wanachama kumi na moja waasisi waliokutana katika ule mkutano wa kwanza
mwezi uliopita. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe wafuatao: Abdallah Rashid
Sembe, Mohamed Kajembe, Victor Mkello, Dhili Mgunya, Ali Mohamed, Abdallah
Mohamed na Mohamed Sadik. Peter Mhando alijitolea nyumba yake kuwa ofisi ya
kwanza ya tawi la TANU mjini Tanga. Mara tu baada ya mkutano huu wazee wa
Tanga wakiongozwa na Makoko Rashid, mwanachama wa zamani wa TAA walianza
kufanya kampeni kwa ajili ya TANU. Chama kilipata msukumo mwingine na
kuongezeka nguvu wakati Sadik Ali Patwa Muasia tajiri alipoingia TANU.
Patwa alikuwa Muislam
wa madhehebu ya Shia. Patwa alikuwa amehamia Tanganyika kutoka Zanzibar
mwaka 1918 baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza. Pale Tanga Patwa
alianzisha kiwanda cha soda na akatajirika. Wakati huo wa zama za ukoloni
wakati Waasia wenzake walikuwa wakiwabagua Waafrika, Patwa alikuwa akikaa
na Waafrika wa rika lake akinywa nao kahawa. Halikadhalika watoto wake
wakawa wanacheza kandanda na vijana wenzao wa Kiafrika katika vilabu vya
Tanga. Hili lilikuwa jambo geni na lisilokuwa la kawaida kutoka kwa familia
ya Kiasia wakati wa ukoloni. Patwa alisaidia harakati za kudai uhuru kwa hali
na mali, na akaifanyia kampeni TANU miongoni mwa jamii yake mwenyewe ya
Kiasia. Wakati wa harakati Nyerere alikuwa akifanyiana maskhara na Patwa
akimwambia, 'Mzee Patwa baada ya kupata uhuru nadhani tukuteuwa uwe balozi
wetu India.' Lakini Patwa hakuiona Tanganyika huru, alifariki kabla ya
uhuru kupatikana.
Baada ya kufungua tawi
la TANU mjini Tanga, uongozi wa chama ulimwalika Julius Nyerere, Bibi Titi
Mohamed, John Rupia na Mbutta Milando kufanya ziara Tanga. Nyerere alifikia
nyumbani kwa Hamisi Heri. Ujumbe huu kutoka makao makuu ya TANU ulipata
makaribisho makubwa yaliyoandaliwa na vyama vya lelemama ambavyo kwa
kawaida vilikuwa vingi sana katika pwani ya Afrika ya Mashariki kutoka
Mombasa nchini Kenya hadi Mikindani, Tanganyika. Kiongozi wa akina mama
hawa mjini Tanga aliyesaidia kuieneza TANU alikuwa Bibi Mwanamwema bint
Sultan, ndugu wa mbali wa mwenyekiti wa TANU Tanga, Hamisi Heri.
Matokeo ya ziara ya
Nyerere Tanga ilikuwa ni kumrudisha Mwalimu Kihere katika siasa. Baada ya
kushindwa kupata nafasi yoyote katika chama, Mwalimu Kihere alipoteza
shauku ya siasa. Nyerere alipokuja Tanga kuifanyia kampeni TANU ndipo
Mwalimu Kihere alikaribishwa kujiunga na chama. Mwalimu Kihere alifahamiana
na Nyerere mwaka 1946 walipokutana Dar es Salaam katika mkutano wa mwaka wa
African Association. Nyerere alipozuru Tanga Mwalimu Kihere alitaka kufanya
dhifa nyumbani kwake kwa heshima yake. Uongozi wa TANU, hususan Hamisi Heri
na Mzee Makoko walikataa kumruhusu Nyerere kuhudhuria dhifa hiyo kwa sababu
Mwalimu Kihere alikuwa hajaonesha kuiunga mkono TANU. Nyerere akitambua utu
uzima wa Mwalimu Kihere, uzoefu na sifa yake ya uongozi katika African
Association, alishauri uongozi wa TANU Tanga usiache fursa ile ipite bure.
Nyerere alitoa hoja kuwa, ilikuwa muhimu kukubali mwaliko wa Mwalimu Kihere
na kutumia fursa hiyo kumuomba arudi kwenye harakati kwa kuwa TANU
ingefaidika kutokana na uzoefu wake alioupata katika African Association.
Kwa ajili ya nasaa hiyo TANU ilikubali mwaliko wa Mwalimu Kihere na Nyerere
alihudhuria dhifa ile nyumbani kwa Mwalimu Kihere pamoja na wanachama
wengine.
Source: http://www.islamtanzania.org/an-nuur3/287/index.html.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !