TIMU iliyoundwa na Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Shaaban
Simba, kuzungumza na Wakristo ili kuondoa tofauti kati ya Wakristo na
Waislamu na kujenga ushirikiano imeanza kazi yake jana.
Timu hiyo imeanza kazi kwa kupeleka waraka maalumu
ulioandikwa na Mufti na kufanya mazungumzo ya faragha na maaskofu ambao ni
viongozi wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini (CPCT).
Waraka huo uliopokewa na Katibu Mkuu wa CPCT, Askofu Dk.
David Mwasota, kwa niaba ya maaskofu wa umoja huo, utajadiliwa na kutolewa
uamuzi.
Alisisitiza kuwa jambo alilolifanya Mufti ni jema na la
kihistoria, ambalo lina nia ya kuleta amani na maelewano ya kudumu baina ya
wanadini nchini.
“Tumepokea wawakilishi wa Mufti (ujumbe wa timu yake) na
waraka maalumu kutoka kwa Mufti mwenyewe. Ujumbe wake una lengo la kutaka
kukutana na sisi, kwa lengo la kuzungumza na kuondoa tofauti ambazo
zimekuwa zikijitokeza.
“Hivyo tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa pamoja na nina
hakika tutaukubali wito wake kwa kuwa una nia njema, kwa maslahi ya nchi
yetu na watu tunaowaongoza,” alisema Askofu Dk. Mwasota.
Kwa upande wake timu iliyoundwa na Mufti imesema, suala la
kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, maelewano, amani na usalama wa jamii
ni wajibu wa kila raia.
Hivi karibuni Mufti Mkuu wa Tanzania, Shaban Simba,
alitangaza kuunda timu hiyo ya masheikh na wanazuoni wa Kiislamu,
itakayotafuta maridhiano baina ya Wakristo na Waislamu ili kudumisha uhuru
wa kuabudu, amani na usalama nchini.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !