MAPEMA wiki hii, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Dk. Willibrod Slaa, alitoa kwa mara ya kwanza ufafanuzi wa ushirikiano uliopo
kati ya serikali na mashirika ya dini yanayojihusisha na sekta ya elimu (MOU).
Huu ni ushirikiano ambao umekuwa ukilalamikiwa kwa miaka kadhaa sasa na baadhi
ya wafuasi wa dini ya Kiislamu kwamba umejaa upendeleo mkubwa.
Kutokana na uzito na umuhimu wa jambo hili, tumelazimika kurudia kile
alichokisema Dk. Slaa ambaye amepata kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu
Tanzania (TEC).
Kwa nini MOU ilizaliwa
Wote mtakumbuka kuwa huko nyuma serikali ilitaifisha shule na nyingi za
madhehebu ya dini. Utaifishaji huo uliendana pia na ardhi, hasa ikizingatiwa
kuwa wakati shule zilijengwa kwenye maeneo ya madhehebu ya dini na papo hapo
kukiwa na kanisa, nyumba za mapadri na kadhalika. Hii ilikuwa hivyo kwa shule
nyingi za kati kama mnavyojua majina yalibadilika sana kati ya 1962 hadi 1965
hivi na ndipo pia darasa la nane lilipofutwa rasmi.
Kwenye miaka ya 1980 madhehebu yakataka yarudishiwe ardhi yao, hasa ambayo
ina majengo mengine ambayo yalikuwa hayahusiani na shule hizo. Mchakato wa
mjadala ulishika kasi mwaka 1986 Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), lilipitisha
azimio rasmi na kumtaka Katibu Mkuu, awasiliane na serikali, kuanzisha mchakato
wa kufanya utafiti na kutenga ardhi ya shule rasmi kutoka kwenye ardhi
inayotumika kwa huduma nyinginezo za madhehebu ya dini.
“Wakati huo mimi nikiwa Katibu Mkuu wa TEC baada ya kupokea rasmi kazi hiyo
Desemba, 1985. Wakati huo pia madhehebu yalidai yarudishiwe Shule zao kwa kuwa
zilikuwa zimegeuka kuwa aibu kwa kukosa ukarabati, na ziko kwenye hali mbaya
sana.
“Serikali ilikuwa imekataa ombi hilo kwa lengo la kuwa Shule hizo zilikuwa
zinawahudumia Watanzania wote bila ubaguzi, jambo ambalo ndilo lilikuwa lengo
kuu la utaifishaji, na sababu ilikuwa bado inaendelelea.
Wakati mawasiliano yalipoanza na serikali wakati huo kupitia Ofisi ya Waziri
Mkuu na Wizara ya Elimu, Serikali iliomba TEC na madhehebu ya dini kwa ujumla,
kama yanaweza kusaidia ukarabati wa shule hizo kwa kuwa zilikuwa kwenye hali
mbaya na hali ya uchumi wa nchi haikuwa nzuri.
Mchakato huo kwa upande wa elimu ulipoanza kulikuwa pia na mgogoro kati ya
serikali na TEC baada ya serikali kuichukua Hospitali ya Bugando kwa utaratibu
huohuo wa kuitaifisha, ikiwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi kwa msaada mkubwa wa
Shirika la Misereor (Shirika la Maendeleo la Baraza la Maaskofu Katoliki la
Ujerumani) toka Ujerumani.
TEC alipowasiliana na wahisani walikataa katakata kujihusisha tena na ujenzi
au ukarabati wa shule au hospitali, vituo vya afya na zahanati kwa kuhofia kuwa
serikali ya Tanzania imekuwa ikitaifisha huduma hizo bila majadiliano ya aina
yoyote na wasingeliweza kuwekeza fedha za walipa kodi wao ( Wajerumani-madhehebu
ya dini yanapata fedha rasmi kutoka kodi ya wananchi) kwa uwiano waliokubaliana
kuendana na idadi ya madhehebu ya dini. Lakini walikuwa tayari kuendelea na
huduma mbalimbali za kusaidia madawa na elimu kwa shule zilizoko bado chini ya
madhehebu kwa kuwa wasingeliweza kuwaadhibu wananchi na watoto.
Kwa kuwa shughuli zote za Bugando zilielekea kusimama na kulikuwa na mgomo
kila siku, kwa madaktari na manesi na watumishi, serikali ikaomba tujadiliane
upya juu ya mambo makubwa mawili:
(a) Utoaji huduma katika sekta za huduma za Jamii,
( b) Kuwa na chombo cha mawasiliano na majadiliano kati ya Ikulu na madhehebu
ya dini na kwa kuwa madhehebu ni mengi wakaomba chombo hicho kiundwe na viongozi
wakuu wa madhehebu yaliyokuwa yanajulikana kwa mujibu wa sheria.
Kuungana kwa Waislamu na Wakristo
Bakwata (hapa sitaki kuingia kwenye mjadala wa kama Bakwata ni chombo
kinachowakilisha Waislamu au la), Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na CCT ( kwa
maana ya madhehebu zaidi ya 60) baada ya mashauriano, tuliunda chombo hicho
kikiwakilishwa na mwenyekiti na katibu wa vyombo nilivyovitaja hapo juu. Uratibu
ulikuwa unabadilika kila mwaka kati ya madhehebu hayo, vivyo hivyo kwa
sekretariati.
Kutokana na utaratibu huo tuliweza kupatia ufumbuzi matatizo yaliyojitokeza
mara kwa mara na ikawa rahisi kwa serikali kuwasiliana na chombo hicho badala ya
kila dhehebu peke yake, na kwa upande wetu pia chombo hicho kikatupa nguvu ya
kujadiliana na serikali.
Kutokana na hali mbaya ya shule za serikali, ikaomba madhehebu ya dini
kusaidia ukarabati wa shule zilizoonekana zitafungwa kutokana na hali hiyo, nasi
kwa upande wetu kwa nia njema ya kuisaidia serikali lakini pia kwa nia ya
kuwahudumia Watanzania tuliwasiliana na wahisani ambao walikazia msimamo wao
kuwa walikuwa hawako tayari kuingia kwenye shughuli za ujenzi wala ukarabati kwa
kukosa msimamo wa wazi na/au wa kisheria wa serikali ya Tanzania kuhusiana na
utaifishaji wa huduma hizo.
Serikali ilipojulishwa, ilichukua hatua ya kuanzisha mchakato mzima wa kupata
suluhu ya jambo hilo.
Ndipo akapewa jukumu hilo, Anne Makinda, wakati huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, na mkutano wa kwanza ulifanyika Kurasini Conference Centre (TEC).
Mikutano ya baadaye ilikuwa leo TEC na kesho CCT kwa kubadilishana. Hii ni kwa
sababu huduma zilizokuwa zinajadiliwa ni za TEC na CCT ( ambao walikuwa
wameathirika na utaifishaji huo).
Hatimaye serikali ilikubali kuwa isingelitaifisha tena, na kwa kuthibitisha
hivyo, ikawa tayari kuwekeana mkatataba na MOU na madhehebu mengine ya dini.
Ndipo tukaanzisha mchakato wa majadiliano na wahisani, ambao katika umoja wao
kati ya dhehebu la Kikatoliki Ujerumani na Kilutheri pia la Ujerumani
tukaanzisha mchakato wa namna bora ya kutoa huduma za jamii. Daima serikali
ilishirikishwa kama mtazamaji katika michakato hiyo, na kwa upande wa Ujerumani
serikali yao nayo ilishirikishwa katika timu za majadiliano.
Hatimaye, makubaliano yalifikiwa, na ndipo kikazaliwa chombo kipya Christian
Social Services Commission (CSSC), chenye sekretarieti yake ( Katibu Mtendaji wa
kwanza akawa Dk. F. Kigadye aliyekuwa Mkurugenzi wa Bugando).
Huduma za kilichokuwa Christian Medical Board (ya TEC na CCT ikavunjwa na
kuwekwa chini ya CSSC) na idara za elimu zilizokuwa chini ya TEC na CCT huduma
zake zikaunganishwa na kuwekwa chini ya CSSC. Ndiyo MOU iliyosainiwa na Askofu
Stanford Shauri wa Dayosisi ya Ruvuma, Mwenyekiti/Katibu Mkuu wa CCT wakati huo
na Askofu Josephat Lebulu, wakati huo Askofu wa Jimbo Katoliki la Same, na
Mwenyekiti wa TEC.
Kwa upande wa serikali kama sikosei aliweka saini Edward Lowassa, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (au Waziri sikumbuki).
TEC na CCT nazo zikawekeana na wahisani mkataba MOU yao ya ndani ili kupata
misaada ya ujenzi, ukarabati na uendelezaji wa huduma zote za jamii. Huduma hizo
zinaendelea hata sasa japo kwa kiwango kidogo baada ya mkataba wa awali
kwisha.
Ninarudia kuwaomba wenzangu, tumetumia muda mrefu sana kujadiliana kwa hisia
za aina mbalimbali. Watanzania hatukuzoea huko nyuma kuulizana dini zetu, wala
kabila wala ukanda.
Haya mambo tukiyaendekeza taifa letu litakuwa hatarini. Tukumbuke kubomoa ni
kazi nyepesi sana, sekunde lakini kujenga tena inachukua muda mrefu na ni kazi
ngumu, na wakati mwingine hata ukifanikiwa huwezi kujenga kama ilivyokuwa.
Nashauri tupende kufanya utafiti zaidi kabla ya kulaumiana au kuhisiana. Kama
mtu hana taarifa za kina awaombe wenye taarifa.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !