NDUGU zangu, haya ni moja ya maandiko yangu muhimu katika kazi yangu ya
uandishi na uelimishaji jamii.
Ni kwa kutambua ukweli kuwa nchi yetu imepatwa na shambulizi la kigaidi.
Imetokea Arusha, ingeweza kutokea popote pale katika ardhi ya nchi yetu.
Tunawapa pole wahanga wa tukio hili. Ni msiba wetu sote. Tuwe sasa na mioyo
ya ustahamilivu. Tusikimbilie kunyosheana vidole. Tuwaache tuliowapa dhamana ya
kuchunguza waifanye kazi yao. Wajibu wetu wa kizalendo ni kutoa ushirikiano.
Naam, kama nchi, tunapitia sasa kwenye kipindi cha majaribu makubwa. Huu ni
wakati wa kuizunguka bendera yetu ya taifa. Ni wakati wa kuonesha umoja,
uzalendo na mshikamano wetu kama taifa. Umoja, uzalendo na mshikamano wetu ni
silaha muhimu na kubwa kabisa Watanzania tumeendelea kuimiliki tangu enzi na
enzi. Ndiyo silaha tunayoendelea kuimiliki hadi sasa.
Tuna lazima ya kupambana hadi risasi ya mwisho kuhakikisha adui hatupokonyi
silaha hii.
Ndugu zangu, hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote, Watanzania wa imani zote.
Tutambue sasa kuwa kwenye safari tunayokwenda kama taifa, mbele yetu kuna
mawimbi makubwa. Kwa pamoja tutavuka, kwa kugawanyika tutazama.
Wahenga wetu walisema; kamba hukatikia pabovu. Watanzania wa imani tofauti
tuna historia ya kuchanganyika na kuishi kwa amani na upendo. Hatuna hulka ya
kubaguana. Tukianza sasa dhambi ya kubaguana, basi, itaendelea kututafuna.
Na siku zote, uzoefu ni mwalimu mzuri. Mathalani, uzoefu unatufundisha kuwa
kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto ni kazi ngumu sana.
Ona, moto ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa
haraka na hata kuteketeza kijiji kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa
hatari ya kucheza na moto.
Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe.
Na ningependa hapa tuyakumbuke maneno ya busara na hekima nyingi kutoka kwa
Bi. Joy Mukanyange.
Huyu alikuwa Balozi wa zamani wa Rwanda nchini Tanzania. Mama huyu aliyatamka
maneno haya miaka 13 iliyopita, takriban miezi sita kabla ya kifo cha Baba wa
Taifa. Bi. Joy Mukanyange alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona.
Ni kama vile alikuwa mtabiri, maana, alichokisema mama yule leo ndiyo
tunaanza kukiona. Siku ile ya Aprili 6, 1999, katika iliyokuwa Kilimanjaro
Hotel, Bi. Joy Mukanyanga aliyatamka haya:
“Naogopa, kwani nimeanza kuona dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa kidini
nchini Tanzania na eneo lote la Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza kusababisha
mauaji ya halaiki kama yale yaliyotokea nchini mwetu mwaka 1994.”
Alisema balozi yule wa Rwanda kabla ya kuendelea kutoa ufafanuzi wa historia
ya Rwanda na matukio yaliyosababisha mauaji yale ya Wanyarwanda ya wao kwa wao.
Ndiyo, Bi Joy Mukanyange alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona.
Na tutafanya makosa makubwa, kama hata sasa, tutajifanya kuwa hatukioni kile
ambacho Balozi Joy Mukanyange alikiona. Watanzania tukubali sasa kuwa tumepatwa
na bahati mbaya sana ya baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za
chuki miongoni mwetu. Kuna wanaotaka tuanze kubaguana kwa misingi ya kidini.
Hili ni jambo la hatari sana. Ni hulka ya mwanadamu, anapokuwa matatizoni
kumtafuta kondoo wa kafara. Mtu mwingine wa kumnyooshea kidole kwa matatizo
yake.
Hali duni ya uchumi wa nchi, hali duni za maisha na umaskini wa watu wetu
isiwe chachu ya kuanzisha vurugu za kijamii.
Maana, taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalani, sisi
Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachaga na wao Wazaramo. Tunasahau kuwa katika
nchi yetu hii hakuna sisi na wao, kuna sisi tu. Tutakapokumbwa na maafa ya
kitaifa watakaoathirika ni sisi, hakutakuwapo na wao.
Hatari kubwa ninayoiona ni tatizo la wengi wetu kuwa na ufahamu mdogo juu ya
dunia tunayoishi sasa, kibaya zaidi, ufahamu mdogo wa historia yetu. Hivyo basi,
kusababisha hali ya kutojitambua kama taifa.
Ndiyo uelewa wa historia ya jamii husika ni jambo muhimu sana. Kiumbe huwezi
kuelewa ya leo, kesho na kesho kutwa kama huelewi ya jana. Kuielewa historia
yako ni kuelewa ulipo na unakokwenda. Historia ni kama maji ya mto, yakipita
hayarudi. Historia ni wakati, ni muda. Kihistoria jana ni sawa na zamani.
Karne nyingi zilizopita wahenga wetu walitafsiri muda kama mkusanyiko wa
matukio ya zamani na sasa. Waliamini kuwa yaliyotokea zamani na yanayotokea sasa
ndiyo yenye kusaidia kubashiri yatakayotokea kesho, yataamua mustakabali
wetu.
Dalili tunazoziona sasa za kupandikiza mbegu za chuki kwa misingi ya udini si
dalili njema. Haya yatatusababishia maafa.
Tuliopata bahati ya kutumia kalamu zetu hatuna budi kuliweka hili hadharani.
Ni wajibu wetu wa kizalendo.
Narudia, hii ni nchi yetu. Katika ulimwengu tunamoishi kuna mamilioni ya watu
ambao hawana nchi.
Wahenga wetu walishiriki katika kuijenga nchi hii, wametutarajia sisi
tuendelee kuijenga na kuilinda heshima na hadhi ya nchi yetu.
Mengine yanayofanyika sasa si tu yanaitia doa nchi yetu, bali, yanaiaibisha
nchi yetu.
Ndugu zangu, hatuna haja ya kubaguana kwa misingi ya dini, ukabila na rangi.
Sisi wote ni Watanzania. Tuna historia ya kujivunia.
Ni historia yetu wenyewe. Kinyume cha baadhi yetu wanavyofikiri au
wanavyotutaka tufikiri, historia yetu haikuanzia enzi za Mwarabu, Mjerumani au
Mwingereza. Historia yetu haikuanzia enzi za TANU wala Afro Shiraz.
Na dini hizi za kimapokeo zinazotufanya sasa tufarakane zimekuja na kuzikuta
dini zetu za asili, na bado tunazo. Na hakika, Afrika hatugombanii
matambiko.
Afrika kila ukoo una tambiko lake, hivyo basi, dini yake. Kamwe hutasikia
Waafrika wanagombania matambiko. Hutasikia Waafrika wakigombana kwa tofauti za
matambiko yao.
Na sisi ni Waafrika. Hii leo mahala ambapo unaweza kuwagawa Watanzania na
hata kufanikiwa kuwafanya wachinjane ni kwenye tofauti zao za imani hizi za
kimapokeo; Uislamu na Ukristo.
Naam; kamba hukatikia pabovu. Tusikubali dini iwe ndiyo penye ubovu kwenye
kamba inayotuunganisha Watanzania.
0754 678 252.
TANZANIA DAIMA.
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !