UTETEZI mkali wa Mufti Sheikh Shaaban Bin Simba kuitetea serikali ya CCM na
hasa Rais Kikwete wiki iliyopita, umenifanya nibakie na swali moja ambalo bado
sijapata jawabu lake la uhakika; ni lini Chama Cha Mapinduzi kimebadilika na
kuwa rafiki ya Waislamu?
Ni swali la muhimu kwa sababu utetezi wake (na hata wa watu wengine)
ulijikita katika suala la “sisi” dhidi ya “wao”. Ulikuwa ni utetezi unaosema
kuwa “sisi” – Waislamu dhidi ya “wao” – wasio Wakristu. Kwa vile hoja hii ya
udini inazidi kusukumizwa katika akili zetu hatuna budi kulizungumzia kwa sababu
kuendelea kuikwepa ni kutoa kibali kuwa pande zenye mirengo ya kidini kuendelea
kutulazimisha kukubaliana na hali iliyopo bila ya kuipinga.
Nina bahati ya kwamba nimekisoma kitabu kizima cha Profesa Hamza M. Njozi
ambacho kilituelezea kwa kiasi historia ya mahusiano ya CCM na Waislamu nchini.
Kitabu hicho ambacho kilipigwa marufuku nchini kinaitwa “Mauaji ya Mwembechai na
Hatma ya Kisiasa ya Tanzania”.
Vile vile nimepata kusoma maandishi mengi ya mmoja wa wanaharakati wa
Kiislamu nchini. Mohammed Said ambaye naye ameandika vitabu na insha kadha wa
kadha ambazo ndani yame ametudokeza (wakati mwingine kwa kirefu) jinsi gani
utawala wa CCM ulivyokuwa ukiwakandamiza Waislamu.
Dk. Njozi ambaye nilipata nafasi ya kufanya naye mahojiano ya kina miaka kama
mitano iliyopita kuhusiana na kitabu chake hicho alinielewesha kwa kirefu sana
jinsi gani utawala wa CCM haukuwa rafiki mzuri wa Waislamu.
Japo watu wengi wanafikiria kitabu cha Njozi kilipigwa marufuku kwa sababu ya
madai yake juu ya mauaji ya Mwembechai binafsi baada ya kukisoma na kukielewa
(hasa ambatisho la barua ya Abu Aziz kwenda kwa Mwanasheria Mkuu) nimegundua
kuwa tatizo kubwa la kitabu hicho ilikuwa ni madai yake makali dhidi ya viongozi
wa CCM na Chama Cha Mapinduzi.
Katika mjadala wa hivi karibuni na Said kwenye mtandao wa JamiiForums.com na
baada ya kusoma maandishi yake mbalimbali ya huko nyuma niliweza kuelewa kwamba
tatizo la Waislamu muda mrefu halikuwa dhidi ya Nyerere tu (hili la Nyerere ni
la siku za karibuni zaidi) bali ulikuwa ni dhidi ya utawala wa CCM.
Kwa muda mrefu viongozi mbalimbali wa Kiislamu wamekuwa na matatizo na
utawala wa CCM, sera zake, uongozi wake, ahadi zake na mipango yake. Kabla ya
miaka hii miwili iliyopita viongozi wengi wa Waislamu walichukulia CCM kama ni
sehemu ya tatizo linalotishia maslahi ya Waislamu.
Hata hivyo, inaonekana matatizo yote ambayo jamii ya Waislamu ilikuwa nayo
katika miongo karibu mitano ya Uhuru wa Tanzania bara sasa yamekwisha. Madhambi
na mambo yote ambayo tuliaminishwa kuwa ni matatizo ya Chama Cha Mapinduzi dhidi
ya Waislamu yamesamehewa na kama maneno ya Mufti hivi karibuni ni ya kuaminiwa
(na sioni sababu ya kutoyaamini) uhusiano mpya wa mapatano kati ya Chama cha
Mapinduzi na Waislamu umeanza. Kuanzia sasa Jamii ya Waislamu imepoteza haki ya
kuilalamikia CCM na serikali yake.
Jamii yetu hii imepoteza haki ya kulalamikia suala la Mahakama ya Kadhi kama
ilivyopoteza haki ya kulalamikia suala la OIC. Mambo yote mawili yameliliwa na
Waislamu kwa muda mrefu na baada ya kurushwa rushwa na kutokupewa majibu kamili
yamebakia kama maneno matamu ya kuvutia. Sasa hivi wale wanaosimamia mambo hayo
hawawezi tena kuyadai kwa nguvu bila kuonekana wako kinyume na serikali.
Kilichobakia ni kutegemea wema na huruma ya CCM kuweza kupatiwa mambo haya.
Lakini haya yanavutia baadhi tu ya Waislamu na wala si Waislamu wote. Kitu
ambacho kinanishangaza sana ni kujaribu kuangalia Waislamu kama watu
wanaoongozwa na hitaji moja tu linalofanana. Sote tunafahamu kuwa hata kwenye
nchi ambazo zina Waislamu wengi kama Saudia, Yemen, Oman, Libya, Misri, Syria,
Iran, na hata Iraq Waislamu huunganishwa na maslahi mbalimbali zaidi ya yale ya
imani.
Mtu yeyote ambaye alichukua muda kufuatilia au anayeendelea kufuatilia mwamko
wa mabadiliko kwenye nchi hizo atagundua kuwa wananchi wa nchi hizo hawaandamani
kwa sababu wanakandamizwa na tawala zenye kuongozwa na makanisa au ambazo
tunaweza kusema kuwa zisizo za Kiislamu; la hasha viongozi wa nchi hizo zote ni
Waislamu na baadhi ya nchi hizo zina mifumo ya Kiislamu ambayo inatawala.
Tungetarajia kwa mfano nchi kama Iran wananchi wake wote wangekuwa hawana
malalamiko yoyote dhidi ya serikali ya Mapinduzi ya Kiislamu. Kwamba, kwa vile
wanaongozwa kwa kiasi kikubwa na mifumo inayoendana na imani yao basi
kusingekuwa na malalamiko ya kudai uhuru zaidi au demokrasia zaidi.
Hili ni kweli hata kwenye nchi kama Saudia ambako tungelazimika kuamini kuwa
maslahi ya kila Muislamu yanalindwa. Lakini haikuwa hivyo; tunakumbuka kuwa
baada ya wimbi la mabadiliko la Tunisia kupamba moto na pale mlipuko wa Uwanja
wa Tahrir ulipozidi watawala wa Saudia kwa haraka wakatangaza kuongeza posho
mbalimbali kwa wananchi wao!
Jawabu ambalo linaweza kutolewa mara moja ni kuwa nchi hizo zote ambazo ziko
katika msuko suko wa kisiasa ziko karibu na Marekani na Israeli na hivyo
wananchi wake ndio maana wameinuka dhidi yake. Hata hivyo, hilo halina ushahidi
kwani yeyote ambaye amefuatilia matangazo ya Al-Jazeera ataona kuwa wananchi wa
hizo wanachodai ni utu wao. Huwezi kuishi kwenye taifa ambalo kuna hali ya
hatari kwa miaka thelathini na ukajiona kuwa uko huru! Huwezi kuishi kwa furaha
katika nchi ambayo watawala wake wanashikilia nafasi zote za utajiri nawe
ukajiona ni sehemu ya jamii hiyo?
Waislamu wa nchi hizo kumbe walitambua kile ambacho naamini ndugu zetu wa
Tanzania walikitambua miaka michache iliyopita kwamba matatizo yao yanahusiana
kabisa na utawala ulioko madarakani. Yeyote ambaye amewasoma vizuri kina Njozi
na Said, Abu Aziz na waandishi wengine wa Kiislamu nchini ataona kuwa walielewa
kile ambacho Wamisri na Wayemen wamechelewa kukielewa. Kile ambacho napendekeza
kuwa Mufti Simba anataka Waislamu wakisahau mara kuwa matatizo yao yanahusiana
na utawala ulioko madarakani - yaani utawala wa CCM.
Barua ya Abu Aziz iliyoko mwishoni mwa kitabu cha Njozi (Nyongeza ya 1) ina
haya ya kusema juu ya CCM na Waislamu “the truth is that the CCM government has
acted arbitrarily and is not alive to the grave situation into which it has
plunged the country. By being biased and allowing itself to be duped by the
Catholic clergy that Muslim preaching was insulting to Christianity, the CCM
government has embarked on a course of action which violates the constitutional
rights of Muslims to propagate religion, is arbitrary and without any regard to
the due process of law.”
Yaani, “ukweli ni kwamba Serikali ya CCM imefanya kiholela na haionyeshi
kujali dimbwi la hatari ambalo imeiingiza nchi. Kwa kuonesha upendeleo na
kukubali kudanganywa na mapadri wa Kikatoliki kwamba mahubiri ya Waislamu yana
kashfu Ukristu, Serikali ya CCM imejielekeza kuchukua hatua ambazo zinavunja
haki za Kikatiba za Waislamu kutangaza dini, ni za kiholela na ambazo hazijali
kabisa kufuata sheria” (Italiki na tafsiri zote toka Kiingereza zangu).
Hiyo ni sehemu ya hukumu kali ya Abu Zaid ambaye sehemu nyingine katika
Waraka mrefu kwa Mwanasheria Mkuu akamka pasipo utata kuwa “The CCM government
has used the criminal justice system to silence Muslims simply because they are
exercising their constitutional right of propagating religion.
The response by the CCM government has been characterised by abuse of power.”
Yaani, “Serikali ya CCM imetumia mfumo wetu wa sheria kunyamazisha Waislamu kwa
sababu tu wanatumia haki yao ya Kikatiba kutangaza dini. Mwitikio huo wa CCM
umeendana na matumizi mabaya ya madaraka”.
Naye Mohammed Said akiandika katika makala aliyoita “Islam and Politics in
Tanzania” anapitisha hukumu hii dhidi ya CCM na Bakwata “The Party is weak, it
no longer commands respect, dignity and enthusiasm it did in the days of yore.
The Party has alienated itself from its founders. The de-Islamisation of the
Party has gone full circle and its Muslim history has been erased. Bakwata has
sided with the government thus failing to uphold Muslim values and principles.”
Kwamba, “Chama (CCM) ni dhaifu na hakina tena heshima, hadhi, na mvuto
kilichokuwa nayo miaka ya nyuma. Chama kimejitenga na waasisi wake. Kuondolewa
kwa kumbukumbu za Uislamu toka ndani ya chama kumekamilika na historia yake ya
Waislamu imefutwa. BAKWATA imechukua upande wa serikali na hivyo kushindwa
kusimamia tunu na kanuni za Kiislamu”.
Sasa haya yote ni ya kweli na ni madai mazito na kama nilivyodokeza hapo juu
ndio sababu kubwa ya kitabu cha Njozi kupigwa marufuku nchini. Watu wengi
wanafikiri kilipigwa marufuku kwa sababu ya kutuelezea na kutuwekea ushahidi wa
yaliyotokea Mwembechai; la hasha. Nina uhakika hata Njozi akiulizwa leo
atakubaliana nami kuwa sababu kubwa ni kuwa kitabu chake kiliweka bayana ile
siri ambayo ilikuwa inajulikana pembeni kuwa CCM inahusika na matatizo ya
Waislamu.
Sasa kama hili ni kweli - na bado sijapata sababu ya kuona kuwa siyo. Huu
urafiki mpya ambao tumeuona hivi karibuni kati ya viongozi wa Kiislamu, makundi
kadhaa ya Waislamu na Chama Cha Mapinduzi umetokana na nini? Ninajiuliza kuwa
kauli ya Sheikh Mkuu Bin Simba kwamba “Misikiti iungurume na wala isikae kimya,
ukimya ufe na yalaani mabaya yote hayo pamoja na dini ya Kiislamu kufanywa
tabaka la chini, tuamke na tushikamane kwa pamoja.” Imetoka wapi?
Au kauli yake hii kwamba “Wanasiasa wanataka kuivuruga nchi kwa visingizio
kuwa wanataka kulinda amani, hivyo Waislamu tumeamua kuvunja ukimya uliodumu kwa
muda mrefu na kuamua kukemea vitendo hivyo” tunaweza kuipa uzito gani hasa
ikizingatiwa kuwa amani ilipovunjwa mwaka 1998 na 2001 Bakwata hawakuwa wakali
kwa serikali kiasi hiki?
Ni wazi kwamba BAKWATA nayo imeamua kujivika taji la kuitetea serikali ya
CCM. Kwa Waislamu wengine hili si jambo geni (kama nilivyoonyesha hapo juu)
kwani mara zote BAKWATA imekuwa ikisimama na serikali ya CCM.
Lakini pia kitu kipya ambacho kimetokea sasa hivi na hasa wakati wa kampeni
ni kuwa hata wale viongozi wa dini ya Kiislamu ambao walikuwa kinyume na
serikali ya CCM walijitokeza na wengi wanaendelea kujitokeza kuitetea CCM mbele
ya umma. Sisi wengine tunajiuliza CCM ilibadilika lini na kuwa rafiki wa
Waislamu?
Ninabakia na majibu kadha wa kadha kubwa ambalo laweza kuonekana ni kuwa
hatimaye matatizo ya Waislamu yamepatiwa tiba ndani ya serikali ya CCM.
Kwamba sera na ahadi za CCM kuelekea 2015 ni bora zaidi kuliko wakati
mwingine wowote na kuliko za chama kingine chochote. Kwamba uongozi wa CCM
umeonyesha kuelewa matatizo ya Waislamu kuliko uongozi wa chama kingine
chochote. Kama hii ni kweli; ina maana ya kwamba.
Ÿ Makosa yote ya CCM ambayo imeyafanya huko nyuma yamefutwa na kusamehewa
rasmi na sasa Waislamu wote waiunge mkono CCM kwa sababu moja tu kuwa hatimaye
maslahi yao kama Waislamu yamepata mtetezi;
Ÿ Madai yote ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi ya Kanisa ambalo tuliaminishwa
kuwa ndilo liko nyuma ya CCM - wengine walifikia kuiita CCM - Catholic Church
Movement hayana ukweli tena - kwa sababu kama CCM bado ni Catholic Church
Movement ina maana Waislamu wanaoiunga mkono CCM wanaunga mkono Kanisa Katoliki;
Ÿ Madai kuwa upo Mfumo Kristo hayana msingi wowote kwa sababu kwa miaka
karibu hamsini Tanzania imekuwa chini ya Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho
kilitengeneza mfumo wa utawala ambao leo unatetewa na kutafutiwa udhuru.
Hii ni kinyume na sisi wengine ambao tunaamini upo “MFUMO FISADI a.k.a MFUMO
CCM” ambao umetunyang’anya haki zetu, kutudhulumu utu wetu na kutufanya tuwe
kama wageni katika nchi yetu.
Ni mfumo ambao umeendeleza umaskini wa Waislamu, Wakristu na Wenye Imani za
Jadi! Mfumo Kristo ni kisingizio, mfumo fisadi ni sababu!
Mfumo huu ambao leo unatetewa kwa nguvu zote unahitaji ujasiri mkubwa sana
kutetewa.
Pamoja na hayo ni wazi tuamini kuwa yumkini kuna sababu nyingine kwani kwa
kipimo chochote kile hakuna mabadiliko yoyote ambayo yametokea ndani ya CCM hata
kuweza kudai kuwa CCM ni bora kwa Waislamu nchini; siyo tu kwa Waislamu lakini
kwa Watanzania wote kwani maslahi ya Watanzania yote yanabeba ndani yake maslahi
ya Waislamu, Wakristu, Wapagani na wasioamini kabisa!
Pendekezo ambalo limetolewa na Shehe Mkuu ambalo yumkini ndio msingi wa
utetezi unaoendelea ni kuwa Rais Kikwete anatetewa kama Muislamu na si kwa
sababu ya CCM. Kwamba, Waislamu wameamua kujitokeza kumtetea Muislamu mwenzao
kwa sababu inaonekana Wakristu na Makanisa yanamshambulia na kushambulia utawala
wake kwa sababu ya Uislamu wake. Kwa maoni ya watetezi wa misingi hiyo wanaona
kuwa akija kiongozi Mkristu basi Wakristu watakuwa na haki ya kumtetea kwa
misingi ya dini yake.
Kuhusu hili la “uenzetu huu” niliwahi kuandika Oktoba 12, 2009 katika makala
yangu niliyoiita “Na Huu ‘Uenzetu huu’ tutashindwa kuwajibishana” nilisema hivi
“Tutaanza kupiga hatua kubwa ya kuwakataa mafisadi pale tutakapoanza kukataa
umoja nao na ushirika nao. Ukisikia fisadi ni Mkristu mwenzako, Muislamu
mwenzako, Mnyakyusa mwenzako, Mhaya mwenzako; vuka hisia zako za “uenzetu” na
umpime kwa matendo yake tu na umpinge vilivyo.
Ni lazima katika fikra zetu tuwe tayari kukataa dhulma, uonevu, wizi wa
utajiri wetu, ubadhirifu, matumizi mabaya ya madaraka, ukandamizaji,
unyanyasaji, unyonyaji wa aina yoyote ile na kwa mahali popote bila ya kujali
unafanywa na nani au kama anayefanya tunafanana naye kwa namna yoyote.
Vinginevyo, mafisadi hawa ambao ni wenzetu ndio kweli mafisadi wenzetu!”
Kwa sababu kama kuna Waislamu wanaomtetea Kikwete kwa sababu tu ya Uislamu
wake (kama ambavyo Mufti anataka tuamini) basi ni wao ambao wanajiweka mahali
pabaya sana;
Sera za CCM zinaweza kusababisha madhara mengi kwa watoto na familia za
Waislamu lakini kwa sababu ni “mwenzetu” basi Waislamu wasilalamike;
Mipango ya maendeleo yaweza isisimamiwe vizuri lakini kwa vile ni “mwenzetu”
Waislamu wasilalamike;
Shule za Kata ambazo zina changamoto nyingi zinaweza kuendelea kufanya vibaya
na kuathiri watoto wengi wa Kiislamu lakini Waislamu wasipaze sauti kubwa kwa
sababu ni “mwenzetu”;
Vitendo vya kifisadi kwenye taasisi za fedha na mikataba mibovu iliyogharimu
mabilioni ya shilingi isilalamikiwe kwa nguvu zote hata kama fedha hizo
zingeweza kutumika kuboresha mahospitali, mashule, kliniki, barabara, usafiri
n.k visipigiwe kelele na Waislamu kwa sababu ya huu “uenzetu.”
Yote haya na mengine mengi yakikubaliwa ni tatizo zaidi. Kwa sababu,
itakuwaje kama kiongozi ajaye wa Tanzania atakuwa ni Mkristu? Na itakuwaje kama
atakuwa ni kiongozi toka nje ya CCM? Itakuwaje kama kuna chama nje ya CCM
ambacho sera na mipango yake ni ya manufaa kwa Watanzania wote na si kikundi
kimoja tu? Je, wale Waislamu wenye kuunga mkono CCM leo hii watakuwa tayari
kukaa na CCM katika upinzani wakisubiri nafasi nyingine?
Hata hivyo hata baada ya kusema hayo yote bado kuna mambo mengi ya kutua
moyo. Viongozi wa Waislamu hawawazungumzii Waislamu wote kwani Waislamu siyo
kundi moja linalofanana kwa kila kitu (homogenous).
Waislamu wa Tanzania kama walivyo Watanzania wengine wana maslahi zaidi ya
kukubaliana kidini. Wakiumwa wanaenda kwenye mahospitali yale yale wanayoenda
Wakristu na Wenye imani za jadi; wakisafiri wanapita barabara zile zile; shule
wanazosoma za umma ni zile zile wanazosoma watu wengine; polisi wanaowalinda ni
wale wale wanaowalinda Watanzania wengine n.k
Kumbe kuna kundi la Waislamu ambalo halijanunuliwa na “huu uenzetu huu”.
Kundi hili ni la vijana na wazee ambao wanatambua kuwa maslahi yao hayana
tofauti na maslahi ya Watanzania wengine. Kundi hili linataka elimu bora kama
wanavyotaka Watanzania wengine; wanataka mafao bora ya uzeeni kama wanavyotaka
Watanzania wengine; wanataka mishahara mizuri kama wanavyotaka Watanzania
wengine na wanataka maisha bora yenye hadhi na utu wa mwanadamu kama wanavyotaka
Watanzania wengine. Kundi hili la Waislamu halikubali ghilba ya kidini kwani
linajua wazi kuwa kufanikiwa kwa Tanzania nzima ni kufanikiwa kwa kila
Mtanzania.
Hili kundi limesoma, halishawishiwi kwa maneno ya kidini tu au ya kiimani
lakini linajuliza maswali ya msingi na linatafuta majibu ya kweli. Kundi hili
linauwezo wa kuchambua mambo kwa kusababisha maswali ya msingi yajibiwe kwanza
kabla halijarukia kwingine.
Linajiuliza kwa mfano kwanini leo tuambiewe tuiunge mkono CCM wakati miezi
michache tu CCM ilikuwa ndio adui yetu? Kwanini tumtetee Kikwete kwa sababu ya
dini yake tu lakini tusihoji uongozi wake? Je ni kweli mfumo Kristo upo au upo
Mfumo Fisadi ambao unaathiri Waislamu kama unavyoathiri Wakritu na Wapagani? Je,
tunaweza kufanikiwa kama Waislamu tu bila kuhakikisha tunafanikiwa kama
Watanzania?
Kundi hili ndilo ambalo unaliona likijitenga na siasa za kidini na kuunga
mkono upinzani wa kweli na haliogopi kujitokeza kufanya hivyo. Kundi hili
halijalishi wachungaji au mapadre wanasema nini kwani linajua kinachotaka.
Kundi hili haliogopi kushirikiana na Watanzania wengine katika kuupinga mfumo
dhalimu wa kifisadi kwa sababu ni katika kufanya hivyo linajitengenezea lenyewe,
na Watanzania wengine mazingira ambapo kila Mtanzania atapata nafasi nzuri ya
kufanikiwa na kuishi kwa uhuru, amani na utu bila kujali rangi, dini, kabila,
mahali, hadhi au nafasi.
Ninaamini kabisa kuwa kundi hili ni kubwa lakini lililo kimya (the silent
majority) na ambalo linatambua bila ya shaka kuwa tatizo la Tanzania linahusiana
kabisa na CCM.
Hili ni kundi ambalo linahofiwa sana na watawala kwa sababu likijitokeza wazi
na kuunga mkono harakati za mabadiliko ya kweli (na nina uhakika litafanya hivyo
siku si nyingi) ambayo yatamnufaisha kila Mtanzania - CCM itakuwa imepoteza
karata ya mwisho ya kuishikilia Tanzania kama paka anavyobeba kitoto chake
shingoni, yaani Udini.
|
|
0 comments:
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !