Sheikh Ponda afungwa kifungo cha nje. - Kitoloho
Headlines News :
Home » » Sheikh Ponda afungwa kifungo cha nje.

Sheikh Ponda afungwa kifungo cha nje.

Written By Msamaa on Friday, May 10, 2013 | 1:17 PM


Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda akisindikizwa na Polisi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, baada kuhukumiwa kifungo cha nje kwa mwaka mmoja. Picha na Venance Nestory

Posted Ijumaa,Mei10 2013 saa 9:7 AM
Kwa ufupi
USULI
Ponda na wenzake 49 walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 18, 2012 na kusomewa mashtaka manne, yote kwa pamoja, huku yeye akikabiliwa na kosa lingine la kula njama, kuingia kwa jinai katika eneo la ardhi, kulikalia kwa nguvu na wizi wa vifaa vya ujenzi mali ya kampuni ya Agritanza vyenye thamani ya Sh59.6 milioni.

Dar es Salaam. Furaha zilitawala jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa kuhukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12 huku wenzake 49 wakiachiwa huru.

Katika kesi hiyo, Sheikh Ponda na wenzake walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh59.6 milioni, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.

Katika hukumu hiyo, Mahakama ilimhukumu Sheikh Ponda kifungo hicho cha nje kwa kosa moja la kuingia kwa nguvu katika eneo hilo la ardhi isiyo yake.

Hukumu hiyo iliwaachia huru washtakiwa wenzake wote baada ya kuridhika kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.

Kabla ya hukumu, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alisema upande wa Jamhuri hauna kumbukumbu za makosa mengine ya jinai dhidi ya mshtakiwa lakini akaiomba Mahakama impe adhabu stahiki kwa mujibu wa sheria.

Akitoa hukumu hiyo iliyosomwa kwa saa 2:12, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa Nongwa alisema: “Kwa kuwa mshtakiwa hana rekodi ya makosa ya jinai na kwa kuwa amekaa rumande kwa muda mrefu baada ya DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka) kuzuia dhamana yake, ni haki kuangalia muda huo.”

“Hivyo Mahakama chini ya Kifungu cha 25(g) cha Kanuni za Adhabu, mshtakiwa unaachiwa kwa masharti ya kutokutenda kosa kwa miezi 12. Unatakiwa ulinde amani na kuwa na tabia njema katika jamii. Ukishindwa hiyo utarudi hapa kwa adhabu nyingine inayokufaa.”

Awali, Hakimu Nongwa alichambua ushahidi wa mashahidi wote 16 wa upande wa mashtaka na 53 wa utetezi akasema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.

Alisema umeshindwa kuthibitisha katika kosa la kwanza, la tatu na la nne, yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa wote na katika shtaka la tano lililokuwa likimkabili Sheikh Ponda na Mshtakiwa wa tano, Sheikh Mukadam Swalehe ambaye ni Kiongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu.

Katika shtaka la pili, Hakimu Nongwa alisema upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa wa kwanza tu, Ponda na kwamba kwa upande wa washtakiwa wengine umeshindwa kuiridhisha Mahakama kuwa walitenda makosa hayo.

Alisema hakuna ushahidi unaoonyesha jinsi washtakiwa hao walivyohusika katika makosa.
Hata hivyo, kwa upande wa mshtakiwa wa tano japo kuna maelezo ya onyo yanayoonyesha kuwa alikiri, lakini akasema maelezo ya onyo tu ya mshtakiwa hayatoshi kumtia hatiani, bali upande wa mashtaka ulipaswa kuweka wazi suala hilo.

Hakimu Nongwa aliponda upelelezi kuwa haukufanyika kwa umakini kiasi kwamba kuna mambo ambayo hayakuwa wazi yaliyoibuliwa na upande wa utetezi, ambayo kama upelelezi ungefanyika kwa umakini, washtakiwa wote wangetiwa hatiani.
“Kuna hisia zinazoonyesha kuwa hawa washtakiwa walishiriki katika makosa haya, lakini sasa Mahakama haiwezi kuwahukumu kwa kushuku tu,” alisema Hakimu Nongwa na kuionya Jamhuri kujiepusha na mashtaka ya kula njama ambayo hata yenyewe inajua kuwa ni vigumu kuyathibitisha.

Wafurika mahakamani
Mahakama ya Kisutu pamoja na maeneo jirani, jana yalifurika watu waliokuwa wakifuatilia hukumu hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika sehemu kubwa ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Magari manane yaliyokuwa yamesheheni askari polisi, mbwa na farasi yalionekana katika eneo la Mahakama hiyo. Mbali ya hao, pia walikuwapo askari kanzu na wengine waliokuwa wamevalia sare.

Wafuasi hao wa Sheikh Ponda walianza kuingia mahakamani hapo saa mbili asubuhi lakini kutokana na askari kuweka kizuizi kwenye lango kuu, wengi waliishia nje.

Baada ya kupata taarifa kuwa Sheikh Ponda ameachiwa, wafuasi hao walishangilia wakisema ‘Takbir! Allahu (Mungu ni mkubwa).’

Furaha ya wafuasi hao, ilisababisha watu wote waliokuwa ofisini katika majengo yaliyo karibu na Mahakama hiyo pamoja na wapita njia kuacha shughuli zao ili kushuhudia.
Baadhi walitoka nje ya ofisi na majengo ili kufuatilia kwa karibu.

Ponda anena
Mara baada ya kuachiwa, Sheikh Ponda alivitaka vyombo vya dola kuacha kutengeneza kesi nzito ambazo inashindwa kuzithibitisha.

“Kuwepo na mfumo thabiti ambao utafanya kesi zisiwe za kubambika au matakwa ya wanasiasa,” alisema na kuongeza kuwa kuachiwa kwake si fadhila, bali ni haki yake kulingana na misingi ya sheria.

Alisema tatizo linalosababisha kesi kuharibika ni mfumo mbovu na ndiyo maana Tanzania inashirikiana na mataifa mengine katika kufanya upelelezi kama lile la Marekani la FBI na kusema ipo haja ya nchi kuwa na mfumo utakaowezesha kuwa na vyombo makini vya upelelezi.

Baada ya kutoka kortini, wafuasi wa Sheikh Ponda waliandamana hadi Msikiti wa Mtambani, Kinondoni ambako alizungumza nao baada ya kupelekwa hapo na gari la polisi.
SOURCE: MWANANCHI.
Share this article :

0 comments:

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

ZILIZOSOMWA SANA.

Followers

Blog Archive

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Proudly powered by Blogger
Copyright © 2011. Kitoloho - All Rights Reserved
Template Design by Creating Website Published by Mas Template